Watu wawili mume na mke wakazi wa Kijiji cha Kilimanjaro, Kata ya Mtumbya mkoani Lindi, Shafii Selemani na Liuza Shafii wamenusurika kifo kufuatia nyumba yao kuteketea kwa moto uliochangiwa na mafuta aina ya Petroli.
Kwa mujibu wa baadhi ya majirani waliojitokeza kusaidia kuzima moto huo bila mafanikio, wameeleza kuwa moto huo ulichangiwa na mafuta aina ya Petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye madumu na kuwekwa ndani ya nyumba yao.
Wameeleza kuwa Shafii ni dereva Bodaboda pia anajihusisha na uuzaji wa mafuta ya Petroli, kwa ajili ya madereva wenzake ili kuwapunguzia tatizo la kufuata huduma hiyo mbali na maeneo yao.
"Moja ya dumu la uzito wa Lita tano likiwa na Petroli lilikuwa wazi bila kufungwa, hivyo harufu yake ilizagaa ndani, ikizingatiwa kulikuwa na moto na kulipuka", amesema mmoja wa majirani aliyefahamika kwa jina la Mashaka.
Mashaka alisema kwamba moto huo umeteketeza mali zote zilizokuwemo ndani, ikiwa ni pamoja na vitanda, Magodoro, chakula, Pikipiki, Nguo na vifaa vingine vilivyokuwepo ndani ya Nyumba yake.