Madeni Yaiweka Njia Panda ATCL



MADENI yanayoliandama shirika la ndege la taifa (ATCL), yanazidi kushika kasi, kufuatia mmoja wa wadeni wake, kupata amri ya mahakama kuzuia moja ya ndege yake, kuondoka nchini Afrika Kusini.

Taarifa iliyotolewa na katibu mkuu wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho, haikueleza kwa kina sababisho la kuzuiwa kwa ndege hiyo.

Ndege iliyozuiliwa, ni aina ya Airbus A220-300. Ilianzia safari yake kutokea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam hadi Oliver Tambo, Afrika Kusini.

Katika taarifa yake hiyo kwa umma, Dk. Chamuriho anasema, “taarifa ambazo serikali imepokea kutoka kwa balozi wetu nchini Afrika Kusini, ndege imezuiwa kwa amri ya mahakama kuu ya Gauteng, jijini Jonesburg.”

Anasema, “serikali kupitia ofisi ya mwanasheria mkuu (AG), inafuatilia suala hilo, ili ndege iliyokamatwa iachiwe mara moja na iendelee na safari zake kama kawaida.”

Kupatikana kwa taarifa kuwa ndege ya ATCL imekamatwa nchini Afrika Kusini, kumekuja takribani mwaka mmoja tokea mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, kuonya serikali kuwa iwapo haitachukua hatua kukabiliana na madeni sugu yanayolikabili shirika, ndege zake, zaweza kujikuta zinakamatwa.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, Aprili mwaka jana, Kubenea alisema, “ATCL inakabiliwa na mzigo wa madeni unaohatarisha ukuaji wake.” Alidai kuwa miongoni mwa wadeni hao, tayari wamefungua shauri katika mahakama mbalimbali duniani, ikiwamo Uingereza.

Aidha, kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja miaka miwili baada ya ndege nyingine ya shirika hilo aina ya Bombedier kukamatwa nchini Canada, Julai mwaka 2017.

Kukamatwa kwa ndege hiyo, kulitokana na serikali kudaiwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Limited (SCEL), iliyokuwa ikijenga barabara kati ya Wazo jijini Dar es Salaam na Bagamoyo, mkoani Pwani.

Serikali iliingia kwenye mgogoro na kampuni hii, kufuatia uamuzi wake wa kuvunja kwa mkataba huo; jambo ambalo lilisababisha SCEL kwenda mahakamani nchini Uingereza.

Katika maamuzi yake, tarehe 10 Juni mwaka 2010, mahakama ya usuluhishi ya migogoro ya kibiashara (ICSID), iliamuru serikali ya Tanzania kulipa kiasi cha dola za Marekani 21 milioni.

Serikali haikulipa deni hilo; mpaka ndege inakamatwa nchini Canada, ilikuwa inapaswa kulipa kiasi cha dola za Marekani 38.1 milioni (Sh. 70 bilioni).

Akizungumzia kukamatwa kwa ndege ya Airbus A220-300, kulikofanyika  jana Ijumaa, Dk. Chamuriho ameomba radhi wasafiri waliokuwa wamepanga kuondoka na ndege hiyo kutokea uwanja wa ndege wa Oliver Tambo kuja Dar es Salaam.

Amesema, serikali inaendelea kuwaomba radhi abiria wote kwa usumbufu uliyotokea. Tunaendelea kufanya mawasiliano ili kuhakikisha ndege iliyozuiliwa inaachiwa huru.

Katibu mkuu hakueleza nani aliyeshitaki ATCL. Hakueleza kiasi kinachodaiwa, hakueleza sababu ya kuwapo kwa deni hilo; na wala hakueleza mkakati wa serikali wa kukomboa ndege iliyokamatwa.

MwanaHALISI limeshindwa kupata kwa ufasaha jina la mdai, kiasi kinachodaiwa na chanzo halisi cha kuwapo kwa deni hilo.

Hata hivyo, kampuni ya ndege ya ATC, inakabiliwa na madeni makubwa yaliyotokana na maamuzi mabovu ya ubinafishaji wa shirika hilo kwa wageni ATCL lilifikishwa hapo kutokana na sera ya ubinafishaji yaliyobuniwa na rais mstaafu Benjamin William Mkapa.

Maamuzi hayo yaliyosababisha uuzwaji wa hisa za shirika kwa shirika la ndege la Afrika Kusini – South Africa Airways (SAA) – yaliingiza kampuni kwenye mzigo mkubwa wa madeni, kufuatia serikali ya Tanzania kuamua kuvunja mkataba wa uuzaji wa hisa zake.

Nyaraka ndani ya serikali zinaonyesha kuwa baada ya kuvunjika kwa mkataba wa ubia – Joint Venture – ATCL liliendelea kuratibu kwa niaba ya serikali, shughuli mbalimbali za urekebishaji wa shirkka.

Mbali na shirika la ndege la Afrika Kusini, wadai wengine wakubwa wa  ATCL, ni pamoja na kampuni ya Wallis Trading Company iliyokodisha ndege aina ya A. 320 kwa ATCL.

Kampuni ya Wallis nayo imeripotiwa kufungua shauri la madai katika mahakama za Uingereza.

Kampuni hiyo ilikodisha kwa ATCL ndege aina ya Airbus ambayo imeingiza hasara ya mamilioni ya dola za Marekani.

Serikali kupitia ATCL iliingia na kampuni ya Wallis wa miaka sita ambako kila mwezi ATCL ilijifunga kulipa kiasi cha dola za Marekani 360,000.

Bei halali ya soko kwa ukodishaji wa ndege ndege mpya na ya kisasa, ni kati ya dola za Marekani 220,000 na 260,000.

“Serikali iliendelea kunyamazia mkataba huu wa kinyonyaji hadi pale walipojulikana kuna baadhi ya viongozi wa juu waliokuwa wakipata mgao wakiwemo maofisa wa wizara ya miundombinu,” kimeeleza chanzo cha taarifa serikalini.

Mtoa taarifa anasema, “kampuni imekuwa ikibeba hasara zisizotarajiwa huku bodi ikipitisha kila kitu bila kujali ipo siku zile zinazoliwa zinaisha muda wake. Inasikitisha. Mwenye ndege kaamua kuichukua na huku akiidai serikali na kampuni takribani dola za Marekani 11.5 milioni.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad