MVUTANO mkali kati ya pande mbili – upande unaowakilishwa na Tundu Lissu na ule wa Jamhuri katika kesi ya kuvuliwa ubunge (Lissu), umeibuka kwenye Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Leo tarehe 15 Agosti 2019, upande wa Jamhuri umeeleza mahakamani hapo kwamba, muda wa kujibu maombi/hoja ya upande wa muombaji (Lissu) wa siku tatu, hautoshi.
Hata hivyo, upande wa muombaji (Lissu) umeieleza mahakama hiyo kwamba, Jamhuri haina sababu ya kuomba muda mrefu kujibu maombi yao na kwamba, siku tatu zinatosha kukamilisha majibu hayo.
Mabishano hayo yameibua mvutano mkali wa kisheria katika pande hizo mbili, kwenye kesi hiyo ya kupinga hatua ya Job Ndugai, Spika wa Bunge kumvua ubunge wa Lissu.
Lissu alikuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, alivuliwa ubunge na Spika Ndugai tarehe 28 Juni 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge.
Lissu, mmoja wanasheria mashuhuri nchini, alifungua shauri la kupinga kuvuliwa ubunge wake, kwenye mahakama hiyo Jumatano, tarehe 7 Agosti 2019, chini ya hati ya dharura.
Kwenye mvutano mahakamani hao, mbele ya Jaji Sirilius Matupa upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili Vincent Tangoh, Wakili wa Serikali Mkuu; Lucas Malunde na Mark Mulwambo.
Mawakaili hao wameiomba mahakama kuwapa siku nane ili kujibu maombi hayo sambamba na kuwasilisha hati ya kiapo.
Katika kesi hiyo, upande wa muombaji (Lissu) unawakilishwa na Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya, Omari Msemo na Fred Kalonga.
Upande wa muombaji (Lissu) umetoa hoja kwamba, siku nane zilizoombwa na Jamhuri ni nyingi kutokana na kwanza; maombi hayo kufunguliwa chini ya hati ya dharura, pili; kiapo kinachoelezwa na Jamhuri hakizui kutojibu maombi hayo ndani ya siku tatu.
Hata hivyo, Jaji Matupa ameahirisha shauri hilo kwa dakika 30 kwa ajili ya kutuoa uamuzi.