Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema anatambua wapo akina baba ambao wanaumizwa na wanawake atawatafutia dawa yake.
“Najua wapo akina baba ambao wameumizwa inafika wakati wakina baba nao wameahidiwa na akina dada wanakubaliana alafu anaachwa. Hiyo nayo tunaitafutia dawa yake ifiki wakati aliyetoa ahadi aitekeleze,” alisema Makonda
Makonda alisema kimsingi kwa mujibu wa sheria ni kosa kutoa ahadi usiyoweza kuitekeleza.
Alisema atatumia mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuuliza nchi zao zinafanyaje kuwashughulikia wanaume ambao wanawaumiza wanawake kwa kuwaahidi kuwaoa alafu wanawaacha.
Makonda alisema wanawake wengi wa jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakilalamikia kuumizwa na wanaume, hivyo wamechoka kutapeliwa kwani wanakuwa na majeruhi moyoni mwao.
Makonda alisema akiwa kama Mkuu wa Mkoa hawezi kuwaongoza watu wenye kuumizwa, hivyo atakwenda kuwashughulikia na kwamba kupitia mkutano huo wa SADC watapata uzoefu jinsi wao wanavyoshughulikia wanaume wanaowaumiza wadada .
“Tunampango wa kukutana na wadada wote walioumizwa na ahadi za kuolewa lakini wakaachwa ili kujadiliana kwa kina namna gani ya kuwashughulikia wanaume hao lakini pia tutajifunza pia kwa wenzetu wa SADC sheria zao zikoje na wanafanyaje kuwashughulikia wanaume wadanganyifu,” alisema
Aliongezea kuwa:”Lengo ni kuepusha wadada wengi wasiingie kwenye mahusiano ya kwenda kuwaumiza lakini pia itasaidia kuondoa zile ndoa za kimya kimya bila kuwajulisha wanawake wao hawa wageni wetu watatuambia huko kwa Mfalme Mswati wanafanya utaratibu gani, Zimbabwe wanafanyaje ili tuone ni njia gani ya kuwaondoa wadada wasiendelee kuumizwa,” alisema Makonda
Aidha, Makonda alisema kuna mpango wa kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo katika mkoa wa Dar es Salaam ili kupunguza utapeli wanaofanyiwa wanawake kwa kudanganywa kuolewa.
“Hii data base itasaidia mwanamke akiambiwa kuwa anaolewa ataingia katika mtandao na kuangalia jina la mwanaume huyo kama ameoa au la na hata itawasaidia wanawake ambao wameolewa ili kuzuia waume zao wasioe kwa siri. Wanawake mkishaolewa washawishini wanaume waje kusajili vyeti vya ndoa,” alisema Makonda.
Makonda alisema licha ya kuanzisha kanzi data hiyo atatumia mkutano huo wa SADC kupata uzoefu kutoka kwa nchi nyingine kufahamu namna gani wanavyokabiliana na utapeli wa aina hiyo.