Malinzi Aomba Kunywa Soda Akijitetea Mahakamani

ALIYEWAHI kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, jana Jumanne, aliendelea kujitetea kwa takribani saa tano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.



Malinzi na wenzake, wanakabiliwa na mashitaka 20 ikiwemo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha ambapo kesi hiyo jana ilianza kusikilizwa saa sita mchana mpaka saa 11 jioni.



Katika kesi hiyo, washitakiwa wengine ni aliyekuwa Katibu wa TFF, Celestine Mwesigwa, Mhasibu Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya ambaye yupo nje kwa dhamana, huku wenzake wakiwa rumande.



Wakati akijitetea, Malinzi aliiambia mahakama kuwa fedha ambazo alikuwa anachukua ni sehemu ya malipo ya fedha alizokuwa ameikopesha TFF.



Aliendelea kuiambia mahakama kuwa fedha hizo hawakuwahi kuandikiana popote na alizitoa kutokana na programu alizoziendesha kama rais na programu zilikuwa endelevu.



Kiongozi huyo wa zamani wa TFF, alifafanua zaidi kuwa yeye si kiongozi wa kwanza kuikopesha TFF kwani hata Ahmed Mgoyi alikuwa akifanya hivyo na kuongeza kuwa, hata mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji ameikopesha Simba takribani Sh bilioni 6, hivyo si ajabu kwake kuikopesha TFF.



Katika ushahidi wake, Malinzi aliiambia mahakama kuwa Mgoyi aliwahi kuikopesha TFF Sh milioni 55 na katika kuthibitisha hilo waliiomba mahakama ipate bank statement ya Mgoyi na TFF, lakini hawakupatiwa.



Aliendelea kuiambia mahakama kuwa fedha ambazo aliikopesha TFF zimeainishwa katika mashitaka yake na aliyekuwa Mhasibu Nsiande Mwanga hakuwahi kusaini fedha ambazo zilitoka CRDB Bank kwa sababu alikuwa mtia saini wa Stanbic Bank.

Malinzi alifafanua kuwa, Shirikisho lilikuwa na akaunti katika Benki za CRDB, NBC, Stanbic na baadaye walifungua DTB.



Katika fedha ambazo aliikopesha TFF ni Sh milioni 13 za kwenye shitaka la 15, Sh milioni 20 (shitaka la 16), Dola 28,650 (shitaka la 18), Sh milioni 4 (shitaka la 19), Dola 24,000 (shitaka la 20) na shitaka la 21 dola 25,000, fedha zote zimetolewa bila ya kuwepo nyaraka zilizoambatanishwa.



Pia fedha hizo zilizoainishwa katika mashitaka hayo zilikuwa na mapungufu kutokana na baadhi ya nyaraka kutoambatanishwa na nyingine kutoonyesha kama zililipwa.



Hata hivyo, Malinzi aliendelea kujitetea na kuomba kuwa ingekuwa vyema kama wangepata taarifa fupi za akaunti za TFF kuweza kupata picha halisi kipindi ambacho alikuwa akitoa fedha.



Katikati ya utetezi wake, Malinzi aliomba apate nafasi ya kunywa soda akidai koo lake kukauka ambapo aliruhusiwa kufanya hivyo.



Kesi hiyo ambayo inaendeshwa na Hakimu Mkuu Mwandamizi, Maira Kasonde, imeahirishwa na itaendelea kusikiliza utetezi Septemba 2, mwaka huu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad