Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amedai wanaolikopesha shirikisho hilo ni wengi, lakini anashangaa yeye kushtakiwa wakati ni jambo la kawaida tangu miaka ya 60.
Amesema kukopa kwa Klabu ya Simba na Yanga pia ni kawaida. Akatolewa mfano Klabu ya Simba ilikopa Sh bilioni Sita kwa Mohammed Dewji ambaye aliwasamehe wakati wa uzinduzi wa uwanja wao wa Bunju.
Malinzi anayekabiliwa na mashtaka ya kughushi na kutakatisha fedha amedai kuwa, aliikopesha TFF kwa nyakati tofauti bila kudai riba na kwamba alilipwa deni kwa mafungu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Utetezi huo aliendelea kuutoa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde.
Mbali na Malinzi, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya.
Akiongozwa na Wakili Richard Rweyongeza, Malinzi alidai taasisi zote za soka, Klabu ya Simba na Yanga, vyama vya soka vya wilaya na mikoa kukopa, hivyo ni utaratibu wa kawaida.
Alidai hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Simba Bunju, Mohammed Dewji alisamehe deni la Sh bilioni sita alizoikopesha Simba kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo usajili.
Alidai utaratibu huo uko miaka mingi lakini yeye ni wa kwanza kushtakiwa kwa sababi hiyo.
Malinzi aliwataja wengine wanaokopesha kuwa ni Ahmed Mgoy, ambaye aliikopesha TFF Sh milioni 55 na Mkurugenzi wa Fedha, Daniel Msangi alithibitisha hilo mahakamani wakati akitoa ushahidi.
Anadai akiwa kama kiongozi na familia ya TFF, aliwajibika kutoa fedha zake ikiwamo kuitumia Dola za Marekani 7,000, timu ya Taifa ‘Taifa Staa’ ilipokwama nchini Zimbabwe.
Alidai kuwa alikamatwa Juni 27, akiwa kwenye usaili kama mgombea urais na kukaa mahabusu ya polisi mpaka Juni 29,2017 aliposomewa mashtaka yanayomkabili kwa mara ya kwanza na kwamba Julai Mosi, mwaka huo alitenguliwa wadhifa wake kama rais.