Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo limeshakamata vyombo vya moto takribani 126, pikipiki zikiwa 87, bajaji 13 na na magari 26 yenye ving'ora na taa sumbufu (Spotlight).
Hatua hiyo imefikiwa baada ya wahusika kukaidi agizo lake la kutofika maeneo ya mjini
pamoja na agizo la watu wenye magari ya aina hiyo kuhakikisha wanatoa vifaa hivyo haraka iwezekanavyo.
Kamanda Mambosasa ametoa taarifa hiyo leo Agosti 13, ikiwa ni takribani wiki moja tu tangu atoe marufuku hiyo, lakini watu wengi wameonekana kukaidi agizo hilo, ambapo amewataka wananchi kuendelea kutii sheria bila shurti.
''Ukisubiri kushurustishwa watu walioandaliwa kukushurutisha tupo, kukuwezesha ili uweze kuzitii sheria husika lakini ukizitii mwenyewe bila kusukumwa ni jambo la heri sana na siku zote wanasema heri ya hiari inashinda kusubiri kutumwa'', amesema Kamanda Mambosasa.
Agizo hilo la kuzuia bodaboda kufika maeneo ya mjini pamoja na wenye magari binafsi yanayoleta taharuki na usumbufu barabarani lilitolewa, Agosti 5 ikiwa ni kipindi cha maandalizi ya kupokea wageni kutoka nchi 15, wataokuja kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.