MKUU wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, ameagiza kuzuiwa kwa mali zote za kampuni ya Green Mails hadi itakapolipa deni la zaidi ya shilingi milioni 36 ilizokuwa ikidaiwa na vijiji 23 vinavyozunguka kitalu cha uwindaji kama mkataba ulivyoagiza.
Kampuni hiyo ilikuwa imekodishiwa kitalu cha uwindaji wilayani Longido tangu mwaka 2013 baada ya kukiuka masharti ya mkataba ikiwemo kushindwa kutoa gawio kwa baadhi ya vijiji jirani, kushindwa kutunza mazingira na uhifadhi wa wanyama pori.
Serikali kupitia Wizara ya Utalii imeifutia kibali cha uwindaji kampuni hiyo tangu jana Agosti 8. 2019.
Mwaisumbe amevitaka vyombo vya ulinzi wilayani humo kuzuia mali zote za mwekezaji huyo zilizopo ndani ya eneo la kitalu cha kitalii cha uwindaji cha Lake Natron East hadi hapo atakapolipa fedha za vijiji hivyo na kupiga marufuku kampuni hiyo kufanya shughuli yoyote ya uwindaji katika wilaya hiyo.
Ametoa agizo hilo leo alipokuwa akipokea pongezi za wananchi wa Kata ya Mndalala kwa Rais John Magufuli na serikali kwa uamuzi wake wa kumuondoa mwekezaji huyo.
Wananchi hao wamempongeza Magufuli, Waziri wa Utalii Hamisi Kigwangala, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo na Mwaisumbe na serikali kwa jumla kwa kumuondoa mwekezaji huyo na kutaka haki yao ya fedha zao za gawio la vijiji zisimamiwe hadi wapatiwe na atafutwe mwekezaji mwingine atakayekidhi matakwa ya sheria na maslahi ya taifa.
Mkuu wa Wilaya Longido Aagiza Kuzuiwa Mali za Kampuni ya Green Mails
0
August 08, 2019
Tags