Mkurugenzi wa Afya nchini Msumbiji (MISAU) Bi. Sheila Lobo de Castro ametangaza kuwa nchi hiyo inaimarisha hatua za usalama wa kiafya katika maeneo muhimu ya mpakani ili kutambua watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya Ebola na kuwaanzishia tiba mapema.
Bi. Sheila amesema hayo kando ya hafla ya mahafali ya wanafunzi wa Taasisi ya Sayansi ya Afya, na kuongeza kuwa wizara ya afya nchini humo imeweka vituo vya ukaguzi wa Ebola kwenye mpaka wake na Malawi na Tanzania, uwanja wa ndege wa kimataifa na bandari za kitaifa.
Amesema watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi ya Ebola wamewekwa karantini kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kiafya, lakini hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshukiwa kuwa na Ebola aliyeingia nchini humo.