Mwana wa kiume wa muasisi wa al-Qaeda Osama Bin Laden, Hamza,amefariki , kwa mujibu wa maafisa wa ujasusi wa Marekani.
Taarifa kuhusu mahala au tarehe ya kifo cha Hamza Bin Laden bado haijawa wazi katika ripoti ya chanzo hicho cha habari.
Mwezi Februari, Serikali ya Marekani iliahidi kutoa dola milioni 1 kwa ajili ya yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kutambua ni wapi alipo.
Hamza Bin Laden, anayedhaniwa kuwa na umri wa miaka 30, alikuwa ametoa ujumbe mbalimbali wa sauti na video akitoa wito wa kufanya mashambulio dhidi ya Marekani na nchi nyingine.
Hamza Bin Laden aliwatolea wito wapiganaji wa jihadi kulipiza kisasi mauaji ya baba yake aliyeuliwa na kikosi maalum cha Marekani nchini Pakistan mnamo mwezi Mei 2011.
Kadhalika alikuwa amewatolea wito watu wa rasi ya Arabia kulipiza kisasi. Saudi Arabia ilimyang'anya uraia mwezi Machi.
Aliaminika kuwa katika kifungo cha nyumbani nchini Iran lakini ripoti nyingine zilisema kuwa huenda alikuwa akiishi katika mataifa ya Afghanistan, Pakistan na Syria.
Marekani kumsaka mtoto wa Osama
Mwana wa Osama bin Laden asakwa na Marekani
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema kuwa nyaraka zilizokamatwa katika uvamizi wa mwaka 2011 katika nyumba ya baba yake ya Abbottabad, Pakistan, zinaonyesha kuwa Hamza Bin Laden alikuwa anaandaliwa kuchukua utawala wa al-Qaeda.
Vikosi vya Marekani pia viliripotiwa kubaini video hii ya harusi yake akimuoa binti wa afisa mwingine wa ngazi ya juu wa al-Qaeda ambayo ilidhaniwa kufanyika nchini Iran:
Baba mkwe wake alikuwa ni Abdullah Ahmed Abdullah au Abu Muhammad al-Masri, ambaye anatafutwa kwa madai ya kuhusika katika mashambulio ya ugaidi ya mwaka 1998 dhidi ya balozi za Tanzania na Kenya.
Al-Qaeda lilikuwa ni kundi lililotekeleza mashambulio mabaya ya ugaidi ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Marekani, lakini hadhi yake kwa sasa imeshuka katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita baada ya kuibuka kwa umaarufu wa kundi la Islamic State.
Alikuzwa katika misingi ya kuichukia Marekani
Ni ishara ya jinsi taarifa chache kumuhusu Hamza Bin Laden kiasi kwamba maafisa hawakuweza kuthibitisha umri wake.
Katika miezi ya hivi karibuni walisema kuwa huenda alikuwa nchini Afghanistan, Pakistan au Iran. lakini hawakuweza hata kusema ukweli hasa ni nchi gani mmoja wa watu ambao Marekani ''inawatafuta sana'' anaishi.
Zawadi ya dola milioni moja kwa yeyote atakayetoa taarifa kumuhusu ilikuwa ni hatua si tu ya uwezekano wa hatari anayoweza kusababisha lakini pia ilikuwa ni ishara ya umuhimu kwa al-Qaeda na propaganda yao