Mtuhumiwa Mauaji Aliyemuua mkewe Kisha Kumchoma Aomba Simu Mahakamani Akatoe Pesa

HAMISI LUWONGO, mtuhumiwa anayedaiwa kumuua na kumchoma moto aliyekuwa mkewe, Naomi Marijani, amezua kioja kingine mahakamani baada ya kuiomba mahakama impatie simu zake ili atoe pesa kwenye akaunti yake na azitumie kuwapatia ndugu zake wamsomeshe mwanaye.



Akizungumza mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Salum Ally, wakili wa serikali, Wankyo Simon, alisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuiomba mahakama itaje tarehe nyingine, ambapo  iliamua kesi hiyo itatajwa tena Septemba 10 mwaka huu.



Wakati kesi yake hiyo imesogezwa mbele, mshtakiwa alisimama na kunyoosha kidole kuomba kuzungumza, ambapo aliruhusiwa na kusema kwamba anaomba pesa zilizo kwenye simu yake azichukue awape ndugu yake ili zisaidie kumsomesha mtoto wake.



“Hakimu nina maombi mawili, ombi langu la kwanza nipewe ‘charge sheet’ maana nimeanza kuiomba muda,  nahitaji niwe na nakala yake. Ombi langu la pili, nina simu zangu nne zipo central na katika hizo simu nne mbili zina laini ambazo zina pesa.  Laini ya kwanza ina milioni nne na zaidi na laini ya pili ina milioni moja na zaidi kwa hiyo ni kama milioni tano na zaidi.


“Naiomba Mahakama inisaidie kupata hizo pesa nimpe ndugu yangu ili iweze kusaidia mambo mengine na ada kwa ajili ya mwanangu maana sijui anaishije kwa sasa,” alisema.



Hata hivyo baada ya kumaliza kuiomba mahakama Wankyo alisimama na kutoa mwongozo kwamba hilo haliwezekani kutokana na sheria inavyotaka.



“Nakumbuka nakala ya hati nilishampa ila haina shida nitampa tena leo, lakini kuhusu kupewa simu ili atoe pesa hilo haliwezekani kwa sababu zilichukuliwa kama vielelezo vya upelelezi, hivyo avumilie tu kwa sababu hatuwezi kumpa simu wala laini mpaka upelelezi utakapo kamilika,” alisema Wankyo.



Wankyo aliiambia Mahakama kuwa aidha ombi lake aliwasilishe kwa njia ya barua akimwomba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhusu kupewa simu, na baada ya hapo mkurugenzi huyo ndiye mamlaka ya kutoa oda juu ya mtuhumiwa huyo kupewa simu na kuweza kutoa pesa zake.



Jambo la kipekee ni pale mtuhumiwa huyo kuonekana kivingine, tofauti na watuhumiwa wengine, kwani alikuwa amefungwa pingu miguuni.



Hivi karibuni, katika mlolongo wa kesi hiyo, mtuhumiwa huyo aliwatisha waandishi wa habari mahakamani hapo akipinga kupigwa picha na akawatishia kuwafanyia kitu kibaya, jambo ambalo hakimu mhusika alilipinga akitaka waandishi hao waachwe ili kutimiza wajibu wa kazi zao
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad