Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, amevunja ukimya na kusema kuwa amechoka kuona na kusikia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), likiendelea kutukanwa na watu waliodai kuwa wana lengo la kuvuruga Uislamu.
Kutokana na hali hiyo, amesema kuanzia sasa hatovumilia wala kuona Bakwata ikinyanyaswa au kuvunjiwa heshima na mtu yeyote.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam katika Baraza la Idd El-Adhaa, lilitanguliwa na swala ya Idd iliyoswaliwa katika Msikiti wa Kibadeni, Chanika jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo.
Mufti Zubeir alisema wapo baadhi ya watu wakijifanya ni wasemaji wa Waislamu nchini, ambapo huzungumza mambo yasiyokuwa na maana yenye lengo la kuwagawa Waislamu.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikiota mizizi ikiwa ni pamoja na kukashifu baadhi ya mambo jambo ambalo si sahihi.
“Kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijifanya kulisema Baraza katika ngazi ya taifa, jambo ambalo halitakiwi kwani Baraza lipo chini ya Mufti hivyo tabia hii naona inazidi kuota mizizi na kuanzia sasa tabia hiyo iachwe,”alisema Sheikh Zubeir.
Alisema ni lazima Bakwata ipewe heshima yake kwani hata mataifa mengine kuna mabaraza na wasemaji wao hivyo ni vema kuheshimu matamko yanayotolewa na mamlaka kwa mujibu wa utaratibu.
“Baraza linaongozwa kwa mujibu wa sheria hivyo, linapotoa tamko lolote linapaswa kutekelezwa na kufuatwa kwani halikurupuki,”alisema.
Alisema kuna minong’ono inayoendelea kuwa baraza hilo linaipotosha Serikali jambo ambalo si kweli na kuanzia sasa hawapo tayari kushuhudia Uislamu ukichezewa na baadhi ya watu wachache.
“Nashangaa baadhi ya watu hawa enzi hizo za Mufti waliopita yalikuwa mambo haya na hasa kuyapinga lakini leo hii wanayapinga kwa kweli nimechoka chokochoko hizi na sipo tayari kuona zikiendelea,”alisema.
Alisema Bakwata ni chombo huru cha kila Muislamu hivyo kama wanaona hawaridhishwi na mienendo yake, ni bora wakatoe malalamiko yao ofisini lakini si kupotosha umma.
Alisema Bakwata haina mwezi wala alama ya aina yoyote hivyo wakitangaza mwandamo wa mwezi wanakuwa wamewasiliana na Kamati Maalumu iliyoundwa ambayo inahusika na uchunguzi wa mwezi.
“Wapo wanaosema Mwezi wa Bakwata, sisi hatuna mwezi inabidi haya matusi yaachwe kwani kamati imekuwa ikiwasiliana na Kenya pamoja na Visiwani Zanzibar hivyo kitendo cha kutukana ni kuwatukana na wenzetu tunaoshirikiana katika hilo,” alisema Zubeir.
Alisema ni vyema Waislamu wakajifunza kutii mamlaka, kujenga umoja na mshikamano kwani ndio utaratibu wa maendeleo ya nchi yoyote ile.
“Acheni kuandika ama kutukana katika mitandao au sehemu zozote kwani sisi tupo tayari kupokea malalamiko, mkisema tuwajibu kwenye mitandao hata sisi tuna watu wanajua kujibu tukitaka watafanya hivyo ila tunatumia busara na hekima,” alisema Mufti Zubeir.
Alisema ni vyema wakati wanasherehekea Sikukuu ya Idd wakarejea kwenye mstari kwani naye yupo tayari kusamahe na amewasamehe wote waliomkwaza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa, Sheikh Khamis Mataka alisema, baraza hilo lipo kwenye mkakati wa kuandaa mfumo maalumu ambao utawafanya waislamu wote kuswali siku moja swala ya Idd.
Alisema kitendo cha kugawanyika na kuswali siku mbili tofauti kinatia doa Uislamu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.
“Unakuta ndani ya familia ndugu wanaswali Idd siku tofauti wengine leo, baadhi yao kesho jambo ambalo likiachiwa litavuruga Uislamu,” alisema Sheikh Mataka.
Alisema licha ya kuwapo kwa tofauti ya taasisi na baraza ni vema kila mtu akatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria badala ya kuleta mifarakano ndani ya jamii na nchi kwa ujumla.
Naye Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma, alisema wamechoshwa na migogoro ya kila kukicha inayoendelea kwenye misikiti mbalimbali nchini.
Alisema wanaoanzisha migogoro hiyo wanafahamika na watambue kuwa haina afya kwa ustawi wa jamii ya Kiislamu na taifa kwa ujumla.
Mruma alisema Bakwata inaagiza kumalizika kwa migogoro hiyo haraka iwezekanavyo vinginevyo wataingilia kati jambo hilo.