RAIS wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amelazwa hospitalini nchini Singapore, amesema Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa, katika taarifa aliyotoa japo hakusema ugonjwa unaomsumbua Mugabe.
“Mugabe yuko hospitali nchini Singapore anakopatiwa matibabu. Tofauti na zamani ambapo rais huyo wa zamani alihitaji matibabu na uangalizi wa mwezi mmoja tu, madaktari wake sasa wamesema atakaa hospitali muda mrefu zaidi, ikiwa ni tangu Aprili mwaka huu alipokwenda kupatiwa matibabu hayo,” amesema Mnangagwa.
Timu ya maofisa imetumwa kwenda Singapore kufuatilia matibabu ya Mugabe ambapo imesema anaendelea vizuri na ataondoka hospitali hivi karibuni.
Kumekuweko na uvumi kwamba mnamo miezi ya karibuni, Mugabe, mwenye umri wa miaka 95, amekuwa hawezi kuzungumza na kwamba hawezi kutembea.