Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam , Paul Makonda amesema atatumia mkutano wa SADC kuuliza nchi zao zinafanyaje kuwashughulikia wanaume ambao wanawaumiza wanawake kwa kuwaahidi kuwaoa alafu wanawaacha.
Makonda aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alizungumzia ujio wa Rais wa Afrika Kusini ambaye atafika kesho.
Alisema wanawake wengi wa jiji la Dar es Salaam wamechoka kutapeliwa kwani wanakuwa na majeruhi moyoni hivyo huwezi kuwaongoza watu wenye kuumizwa.
“Tunampango wa kukutana na wadada wote walioumizwa na ahadi za kuolewa lakini wakaachwa ili kujadiliana kwa kina namna gani ya kuwashughulikia wanaume hao lakini pia tutajifunza pia kwa wenzetu wa SADC sheria zao zikoje na wanafanyaje kuwashughulikia wanaume wadanganyifu,” alisema
Aidha, alisema wanampango wa kusajili na kuweka orodha ya kila ndoa zitakazofungwa katika mtandao lengo ni kuwakamata wanaume ambapo ni wadanganyifu kwa wanawake zao.
“Hii data base itsaidia mwanamke akiambiwa kuwa anaolewa ataingia katika mtandao na kuangalia jina la mwanaume huyo kama ameoa au la na nyie wanawake mkishaolewa washawishini wanaume waje kusajili vyeti vya ndoa,” alisema Makonda.