Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema, mapinduzi ya viwanda ni lazima ili Afrika ijikomboe kiuchumi.
Amesema, kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo Afrika kwa sasa mchango wa bidhaa za viwandani za Afrika kwenye uchumi wa dunia ni chini ya asilimi 3.
Rais amesema jijini Dar es Salaam kuwa, ingawa kuna msukumo wa kukuza sekta ya viwanda, kiwango cha ukuaji wa sekta hiyo bado ni kidogo sana.
"Kwa sababu ya kutokuwa na viwanda, nchi za Afrika zimebaki kuwa masikini.Tumeendelea kuwa wazalishaji wa malighafi kwa ajili ya mataifa yenye viwanda, na huo ndio ukweli. Na kwa kuwa malighafi hizi hazijaongezewa thamani tunaziuza kwa bei ndogo sana," amesema.
Ameyasema hayo wakati anafungua Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kwa mujibu wa Rais, kwa sasa inakadiriwa kuwa asilimia 62 ya mauzo ya nje kutoka barani Afrika ni bidhaa ghafi na kwamba, hicho ni kiwango kikubwa kabisa ikilinganishwa na mabara yote.
Amesema, nchi za Afrika zimeendelea kuagiza bidhaa za viwandani kutoka nje zinazotokana na malighafi zinazotoka Afrika hivyo hakuna urari mzuri wa biashara kwa bara hili.
Rais Magufuli amesema, bidhaa zinazootoka nje ya Afrika zinauzwa kwa bei kubwa, na waamuzi wa bei ni wenye viwanda hivyo kumaanisha kuwa Afrika haina nguvu ya kupanga bei ya bidhaa ghafi au za viwandani hivyo haina nguvu kwenye soko.
Amesema, sekta ya viwanda inachangia 10% ya pato la taifa la nchi za SADC na inachangia asilimia 11 tu ya pato la jumuiya hiyo.