Rais wa Chad atangaza hali ya dharura
0
August 19, 2019
Rais wa Chad, Idriss Deby ametangaza hali ya dharura nchini humo mara baada ya kutokea mapigano makali huko mashariki mwa Chad kati ya Wakulima na Wafugaji ambayo yamepelekea vifo vya watu zaidi ya 50.
Kiongozi huyo pia amesema kuwa serikali itapeleka vikosi vya jeshi ili kuhakikisha usalama kwenye eneo hilo ambalo limekumbwa na mapigano.
Rais Deby alitangaza hali ya dharura ya kitaifa siku ya Jumapili katika majimbo mawili ya mashariki nchini humo baada ya mapambano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha vifo vya watu wengi mwanzoni mwa mwezi huu.
Taarifa kutoka ofisi ya rais ilieleza kuwa hali ya dharura kitaifa itakuwepo kwa muda wa miezi mitatu katika maeneo ya Sila na Ouaddai mahala ambapo watu 50 wamekufa tangu Agosti 9 katika mapigano kati ya wafugaji na wakulima.
Mashariki mwa Chad ni eneo lililopo kwenye mzunguko wa ghasia kati ya wafugaji ambao wengi ni kutoka kundi la kabila la Zaghawa mahala ambapo Deby anatokea na baadhi ya wakulima wanatoka jamii ya Ouaddian.
Hata hivyo, Ukame na ongezeko la watu vimechangia pakubwa mzozo kwenye eneo hilo pamoja na mmiminiko wa silaha holela kutoka maeneo jirani yenye mzozo kwa jumla vimechangia vifo kuongezeka.
Tags