Usajili wa mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Robin van Persie kujiunga na Manchester United uliwashtua watu kutokana na wengi wao kuamini nyota huyo hawezi kuhamia timu pinzani ya Arsenal na kama angehama basi ingekuwa nje ya England.
Baada ya Robin van Persie ,36, kujiunga na Manchester United 2012 , uhamisho huo uliwakwaza mashabiki wa Arsenal na wakamchukia mchezaji huyo.
Mholanzi huyo sasa ametaja sababu ya kuamua kuhamia Man United.
"Unaweza kulinganisha mimi nilivyokuwa (Arsenal) ni kama mtu aliye katika ndoa, mimi na mke wangu (Arsenal) tulioana kwa miaka nane, baada ya miaka nane mke wangu akawa amechoka na mimi, hiko ndicho kilichotokea" alisema Van Persie kupitia kituo cha Televisheni cha BT Sports
"Kama Arsenal hawakukupa ofa mpya unaweza kuwa na mawazo tofauti katika hilo, ukweli ni kwamba sikuwa nimepewa ofa mpya na Arsenal" alisema
Van Persie anasema kuwa baada ya hapo, alikuwa na chaguzi tatu, ambazo ni kwenda kucheza nje ya Uingereza ambapo dili hilo lilipotea, na zingine mbili ni kwenda Man City au Man United, na ndipo akachagua kwenda United