Sababu Tatu za Kisheria za Kumnyima Urithi Mrithi Halali
0
August 25, 2019
Warithi halali ni pamoja na watoto wa marehemu na wake/mke wake halali. Kanuni ya 31 Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali Namba 436/1963 inazitaja sababu 3 ambazo mtoa wosia anaweza kuzitumia kumnyima mrithi halali haki ya urithi kama ifuatavyo ;-
MOSI, ikiwa mrithi amezini na mke wa mwenye kutoa wosia. Mathalan, mtoto wa kiume amezini na mke wa baba yake.
PILI, ikiwa mrithi amejaribu kumuua au amemshambulia au kumdhuru mtoa wosia au amefanya hivyo kwa mke wa mtoa wosia.
TATU, ikiwa mrithi bila sababu za msingi hakumtunza mtoa wosia katika shida ya njaa au ugonjwa.
Ipo sababu nyingine ya kuwa mrithi ameharibu mali ya mtoa wosia, lakini sheria inasema sio sababu ya kumnyima bali apewe halafu kile alichoharibu kikatwe kwenye mgao wake.
Basi, nje ya hizo sababu huwezi kumnyima mrithi halali urithi. Haijalishi mali ni zako, watoto ni wako na kila kitu ni chako.
Na hii ni kwasababu WOSIA ni zao la sheria na hivyo kuandaliwa kwake, kuhifadhiwa kwake, na kutekelezwa kwake ni lazima kufuate sheria. Wosia sio suala la matakwa ya mtu 100% kama wengi wanavyojua, bali matakwa ya sheria kwa karibia 100%.
HATUA 2 ZA KUMNYIMA URITHI MRITHI HALALI.
Ikiwa ni halali kwa vigezo hivyo hapo juu kumnyima mrithi halali urithi basi mtoa wosia kabla hajafanya hivyo ni lazima atekeleze haya mawili ;-
KWANZA, awe amempa nafasi ya kujitetea mrithi anayelenga kumnyima. Hata hivyo, hili si lazima kwa mujibu wa maamuzi katika kesi ya PAULO FERDINAND vs F. BIGUTU(1968) HCD Na. 29. Anaweza kumpa nafasi ya kujitetea kabla hajafa au asimpe.
PILI,ikiwa ataamua kumnyima/kuwanyima ni LAZIMA wosia uwe umeeleza sababu za kwanini mrithi/warithi wamenyimwa. Hii ni lazima kwa mujibu wa kanuni ya 34-39 ya Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali Namba 436/1963.
Ni lazima mtoa wosia/marehemu awe ameeleza katika wosia wake sababu za kwanini fulani na fulani ameamua kuwanyima.
Nini matokeo ikiwa mtu/watu wamenyimwa urithi katika wosia na sababu hazikuelezwa.
Kanuni ya 38 ya Sheria ya Wosia(1963),Tangazo la Serikali Namba 436/1963 inatujibia . Inasema kuwa ikiwa mrithi halali amenyimwa urithi katika wosia, na wosia huo haukueleza sababu ya kumyima au umeeleza sababu lakini zisizokuwa za msingi, kwa maana si zile zinazotajwa na sheria(tulizoona hapo juu), basi wosia huo UNAVUNJWA.
Nini matokeo ya kuvunjwa kwa wosia.
Kanuni hiyohiyo inasema kwamba wosia unapovunjwa basi mali zote zinaanza kugawiwa upya kama vile ambavyo marehemu angekuwa amefariki bila kuacha wosia.
Ni upi utaratibu wa kugawa mali upya kama marehemu hakuacha wosia.
Kama marehemu alikuwa mkristo Sheria ya Urithi ya India ya 1865 ( Indian Succession Act 1865) itatumika kugawa mali zake. Ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha sheria hiyo mgao utakuwa hivi ;-
MOSI,kama mume amefariki na akaacha mjane na watoto basi moja ya tatu ( 1/3) ya mali zote za marehemu zilizo kwenye mirathi anatakiwa apewe mke wake(mjane). Mbili ya tatu( 2/3) ya mali hizo zote itaenda kwa watoto wake wote.
PILI, kama hakuna watoto walioachwa na marehemu katika familia husika lakini kuna mjane,mali ya marehemu hugawanywa katika mtindo ambao ndugu hupewa nusu (1/2), na mjane hupewa nusu ya mirathi ya marehemu(1/2). Hii ni sawa kwa sawa.
N.k., n.k. nk.
Kama marehemu alikuwa mwislamu basi sheria ya kiislam(Quran na Hadith) vitatumika kugawa mali zake.
Kadhalika, kama marehemu hakuwa mwislam wala mkristo bali mtu wa mila basi sheria ya kimila ya THE LOCAL CUSTOMARY LAW (DECLARATION) ORDER 1963 itatumika kugawa mali zake sambamba na taratibu za mila za kabila/koo yake.
Nani ana mamlaka ya kugawa mali upya.
Kanuni ya 39 ya Sheria ya Wosia(1963) inatujibia kuwa wana ukoo wanaweza kufanya hiyo kazi kama kuna maelewano, au mahakama yenye mamlaka.
Nisisitize kuwa WOSIA au MIRATHI ambayo haikufuata au haikurandana na sheria inavyotaka ni BATILI.
Na zaidi, ni kweli mali ni zako, watoto ni wako, na kila kitu ni chako ila zingatia kuwa WOSIA na taratibu za MIRATHI sio zako, ni za sheria na lazima utii, au ujiandae WOSIA wako kutofuatwa baada ya kifo chako.
MWISHO lakini si kwa umuhimu, makala haya hayamlengi yeyote au tukio lolote lililotokea katika jamii yetu hapo nyuma, hivi karibuni, au hapo baadae.
Tags