Safari za mabasi masaa 24 kwa Baadhi ya Mikoa zasitishwa
1
August 02, 2019
Jeshi la Polisi nchini limezuia safari za saa 24 za mabasi kwa baadhi ya mikoa kwa sababu ya kiusalama na kuwataka wamiliki wa mabasi hayo kuzingatia maagizo yaliyotolewa ili kulinda usalama wa wananchi.
Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 2 na Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo, Liberatus Sabas ambapo amesema licha ya kuruhusu mabasi yote nchini kutembea usiku bila kulala sehemu yoyote, Jeshi la polisi limebaini kuna baadhi ya maeneo zoezi hilo limebidi lisubiri kidogo ili wajipange kwa ajili ya usalama na watakapojiridhisha safari hizo zitaendelea kama kawaida.
Sabas amesema mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi hayataruhusiwa kutembea saa 24 kutokana na sababu za kiusalama.
Kamishna Sabas amesema zuio hilo litahusu pia mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea wilaya mbalimbali za mkoani Tabora ambayo yatalazimika kusimama Tabora Mjini na baadaye kuendelea na safari wilayani.
Amesema mabasi yanayotoka mikoa ya Kagera, Katavi, Kigoma kwenda Dar es Salaam yataruhusiwa kutembea saa 24 kama kawaida kutokana na eneo la Morogoro na Dar es Salaam kuwa salama wakati wote.
"Mabasi haya yalikuwa yakitoka kwenye mikoa hiyo yalikuwa yanalala Morogoro, lakini kutokana na hali nzuri ya kiusalama yataendelea na safari hadi Dar es Salaam," amesema Kamishna Sabas.
Amesema mabasi yanayotoka Dar es Salaam kuelekea katika mikoa hiyo yatalazimika kulala wilayani Kahama kisha kuendelea na safari
Tags
Mbona umesahau kusitisha safari za mabasi ya njombe na Songea, kutokana na ukweli kwamba maeneo ya njombe yana ukungu mzito sana usiku ambao ni hatari. Halafu maderva kuendesha usiku barabara za milima ya njombe hadi Songea yenye kona nyingi tena usiku! Tukumbuke zamani magari ya abiria yalikuwa yakisafiri usiku na na kulikuwa na ajali chungu nzima na ndio yakapigiwa marufuku kusafiri usiku. Sasa mweshimiwa waziri wewe unataka yasafiri usiku kama zamani, je ajali za barabarani zilizokuwa zikitokea usiku umezitumbua? Kwanini umependelea usiku dhidi ya mchana?
ReplyDelete