Mo Dewji |
BILIONEA na Mwekezaji wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji amefichua mafanikio makubwa iliyopata klabu hiyo msimu uliopita imemfanya aongeze bajeti mara mbili na nusu na ile iliyopita kwa msimu huu wa mwaka 2019-2020.
Kwa msimu uliopita Simba inadaiwa ilikuwa na bajeti ya Sh 1.3 bilioni zilizoisaidia kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea taji la Ligi Kuu kwa mara ya pili.
Lakini akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Mo alisema ameyaona mabadiliko makubwa ndani ya kipindi cha msimu mmoja, kitu kilichomfanya azidi kuweka nguvu ya kuwekeza zaidi ili kufikia kuwa klabu kubwa Afrika.
“Kuwekeza kwangu ndani ya msimu mmoja na kufanikiwa kusajili nyota mbalimbali ndani ya klabu hiyo kumekuwa na mafanikio makubwa sana katika ligi ya ndani na nje ya nchi hii ni moja ya mafanikio,” alisema na kuongeza;
“Miaka mitano iliyopita, watu walipoteza kabisa hamu ya kuifuatilia Simba, wengi wao walikimbilia kuangali Ligi Kuu ya England, lakini sasa mambo ni tofauti kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata na hii imenipa nguvu.
“Msimu uliopita tuliweka nguvu zaidi, tukawaleta wachezaji wakubwa wa kimataifa, tukatengeneza mfumo wa kusaka wachezaji ‘scouting’ pamoja na kumpata kocha,” aliongeza MO aliyedai kwa sasa timu yao haina haja ya kufanya matangazo makubwa kuwaita mashabiki kwenda kuisapoti katika michezo yao wamekuwa wakienda wenyewe kutokana na ubora wa kikosi ikiwa ni sambamba na matokeo mazuri inayopata.