By THOMAS NG'ITU
HATIMAYE kimeeleweka. Timu ya taifa ya Tanzania kwa Wanawake U20, Tanzanite mchana huu imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Soka ya Nchi za Ukanda wa Kusini wa Afrika (Cosafa Women U20) kwa kuitungua Zambia kwa mabao 2-1.
Ushindi huo mbali na kuwapata taji hilo Tanzania iliyoalikwa tu kwenye michuano hiyo, lakini pia imelipa kisasi kwa wapinzani wao waliokuwa kundi moja la B na kuwachapa idadi kama hiyo katyika mechi ya kukamilisha makundi zikiwa zote zimefusu nusu fainali.
Katika mchezo wa mchana huu uliopigwa kwenye Uwanja wa Wolfson, mjini POrt Elizabeth, nchini Afrika Kusini kikosi cha Bakari Shime, kilianza kupata goli dakika 24 kupitia kwa Opa Clement Sanga aliyetumia vizuri nafasi akiwa ndani ya boksi baada ya kipa wa Zambia kujichanganya na mpira uliokuwa unaambaa langoni mwake.
Hata hivyo Wazambia ambao timu yao ya wakubwa kwa wanawake inajiandaa kuvaana na wenyeji Zambia katika Fainali nyingine ya Cosafa Senior Women 2019 ilichomoa bao mara baada ya kipindi cha pili kabla ya Protasia Mbunda kufunga bao la pili na la ushindi dakika 84 kwa shuti kali akiwa yupo nje ya 18 na mpira ulienda moja kwa moja wavuni.
Goli hilo liliwanyong'onyesha wachezaji wa Zambia, kutokana na kusalia dakika 6 mpira kumalizika kwani wachezaji wa Tanzania walionyesha kutokuwa na presha.
Kilichofanywa na Tanzanite ni kama marudio ya wadogo zao wa Serengeti Boys ambao mwaka jana walialikwa kushiriki Cosafa U17 na kubeba taji kwa kuwafunga Angola katika fainali ikiiwa ni siku chache tangu walipowafunga kwenye makundi.