TEF yataka majeruhi ajali ya moto Morogoro washitakiwe


Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kushtushwa na taarifa za vifo vya Watanzania zaidi ya 60 walioungua moto wakati wakichota mafuta kutoka katika lori lililopata ajali eneo la Msamvu, Morogoro, jana Agosti 10, 2019 likitaka waliojeruhia kushitakiwa watakapopona majeraha yao.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana usiku Jumamosi na Kaimu Mwenyekiti Jukwaa hilo, Deodatus Balile ilisema vifo hivyo vimetokana na tabia mbaya iliyojengeka kwa baadhi ya watu kuchukulia ajali kama fursa ya kujipatia mali kwa njia haramu iliyoanza miaka ya hivi karibuni.

“Tumeshuhudia picha za watu waliofariki kwa kuungua moto zikirushwa kwenye mitandao ya kijamii kinyume cha maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na upashanaji habari. Tunakemea tabia hii na kuitaka jamii iache mara moja tabia hii ya kinyama isiyo ya utu,” alisema Balile.

Balile pia alizungumzia watu zaidi ya 70 waliojeruhiwa katika ajali hiyo akisema wakipona wajiepushe na tabia hii ya uporaji.

“Ikilazimu, wote watakaopona katika ajali hii washitakiwe kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwao na wengine kuwa ikitokea ajali tunapaswa kusaidia majeruhi na kuokoa mali zao badala ya kupora,” alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad