Tiko: Starehe yangu ni kula na kulala


NI Jumamosi nyingine tunakutana tena mpenzi msomaji wa safu hii nzuri ya My Style inayokuletea mastaa mbalimbali wakielezea maisha yao na vitu wanavy-ovipenda.  Leo tunaye msanii wa filamu na muziki wa Bongo Fleva,ambaye anaeleza anavyoishi kuanzia siku inapoanza mpaka inapomalizika, ungana naye kwenye mahojiano yake hapa chini.

My Style: Kwanza mashabiki zako wangependa kujua filamu ulizowahi kucheza mpaka sasa.

Tiko: Zipo nyingi lakini baadhi ni The Living Ghost, Devel Soul, Limbwata na nyingine nyingi.

My Style: Kwa upande wa muziki je, una ngoma ngapi mpaka sasa?

Tiko: Ninazo ngoma zaidi ya tano kama vile, Too Much, Washa, Lambalamba, Funga Virago, Niache na nyinginezo.

My Style: Ratiba yako kwa siku ikoje yaani kuanzia asubuhi unapoamka mpaka jioni?

Tiko: Nikishtuka asubuhi nikiwa bado kitandani kwanza naanza na kuangalia kwenye simu yangu kinachoendelea, baada ya hapo naenda chumbani kwa mwanangu kumwangalia kama yupo salama ndipo mambo mengine yanaendelea.

My Style: Ni kitu gani ambacho unakipenda sana na ndiyo starehe yako?

Tiko: Starehe yangu kubwa ni kula na kulala hivyo muda mwingi napenda kukaa nyumbani kwangu na kupika chakula kizuri baada ya hapo nalala kama sina kazi ya kutoka siku hiyo.

My Style: Mastaa wengi wanapenda kujirusha, vipi kwa upande wako unapenda kujirusha viwanja gani?

Tiko: Sina viwanja maalumu kwa sababu hata hivyo mimi siyo mtu wa kupenda viwanja kivile.

My Style: Shopping zako za nguo huwa unafanyia wapi na shilingi ngapi?

Tiko: Sina sehemu maalumu ya kufanya shopping wala siwezi kusema natumia shilingi ngapi kwa sababu nikiona kitu kizuri sehemu yoyote nanunua huwa sina siku maalumu ya shopping.

My Style: Unavaa nguo za mitumba?

Tiko: Ndiyo navaa kwa sababu naamini kitu kitakachonipendeza ndicho hicho nitakachokivaa.

My Style: Vipi kwa upande wa viatu, unanunua wapi na bei yake shilingi ngapi?

Tiko: Viatu vyangu vinatoka Marekani moja kwa moja na vinaanzia dola 300 (Sh 689,730) na kuendelea na yote haya anasababisha mpenzi wangu hivyo huwa sinunui viatu hapa Bongo.

My Style: Matumizi yako kwa siku ni shilingi ngapi?

Tiko: Inategemea na mizunguko kama niko nyumbani naweza kutumia shilingi elfu kumi au ishirini inategemea na siku hiyo umeamkaje na kiasi cha fedha kilichopo mfukoni maana siku nyingine naweza kutumia hata laki moja.

My Style: Vipi kwa upande wa nywele unatumia gharama gani?

Tiko: Huwa natumia hela kidogo tu maana mimi siyo mpenzi wa mawigi yaani siyo mtu wa kununua manywelenywele.

My Style: Msanii gani Bongo anayekuvutia kwa staili ya mavazi yake?

Tiko: Sijaona maana wanajikongoja na bado tunapambana.

My Style: Unatembelea gari aina gani?

Tiko: Sina gari nina kausafiri lakini siwezi kutaja ni aina gani.

My Style: Gari la ndoto yako ni lipi?

Tiko: Kabla sijakua nilikuwa natamani sana gari aina ya Rav4 hivyo nitaanza na hilo halafu yatafuata magari mengine mazuri ambayo nikishuka au nikikatiza nayo mtaani kila mtu anashtuka.

My Style: Unatumia losheni aina gani?

Tiko: Situlii kwenye losheni aina moja, mara nyingi natumia mafuta ya nazi na glycerin ikitokea nimepata chunusi basi huwa natafuta losheni kama Nivea.

My Style: Asante sana kwa ushirikiano.

Tiko: Karibu sana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad