Ole Nasha amtaka mkurugenzi kumlipa mhandisi wa manispaa ya Bukoka
0
August 06, 2019
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Morris Limbe kumlipa fedha Mkandarasi anayekarabati shule ya Sekondari Bukoba ili aweze kuendelea na kazi na kukamilisha ukarabati huo kwa wakati.
Ametoa agizo hilo mkoani Kagera wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema kuwa wizara hiyo ilishapeleka fedha zote za ukarabati huo kiasi cha shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa mkandarasi huyo amelipwa kiasi cha shilingi milioni 32 tu.
“Fedha zilishaletwa zote na wizara shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa Mzinga wamelipwa shilingi milioni 32 tu kati ya milioni mia mbili na zaidi walizotakiwa kuwa wamelipwa mpaka sasa, hivyo Mkurugenzi wa manispaa dirisha likifunguliwa hakikisha Mzinga wanapata fedha ambazo wanadai,”amesema Ole Nasha.
Amesema kuwa ukarabati wa shule hiyo unaoendelea umechelewa kukamilika licha ya fedha hizo kupelekwa mapema, mkandarasi amechelewa kuanza kufanya ukarabati huo ingawa kasi si mbaya kutokana na kuanza mwezi wa tano.
Aidha, Ole Nasha amesema kuwa shule hiyo ina nafasi finyu ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi mia saba waliopo, hivyo amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Leonard Akwilapo kuwasiliana na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) ambao wana eneo karibu na shule hiyo ili waweze kulitoa kwa ajili ya upanuzi.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Bukoba, Raymond Mutakyawa amesema kuwa ukarabati wa shule hiyo ulikuwa ufanyike kwa siku sabini na tano na ulipaswa kuwa umekamilika mwishoni mwa mwezi wa saba, lakini ulisimama kutokana na kukosa fedha za kununua vifaa kwa ajili ya kazi hiyo baada ya mfumo wa malipo kufungwa kabla ya fedha hizo kulipwa kwa mkandarasi.
Shule ya Sekondari ya Bukoba inafanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya kuharibiwa na tetemeko la Ardhi Septemba 10,mwaka 2016 lililoukumba Mkoa wa Kagera ambapo baadhi ya kuta zilianguka na majengo mengine kupata nyufa na baadaye kuezuliwa na upepo mkali.
Tags