Wawakilishi wa Ujumbe wa SADC wametembelea viwanda Vitatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na Chalinze kikiwemo kiwanda kikubwa za kuzalisha malumalu(Tiles) kwa Afrika Mashariki na Kati cha KEDA.
Akizungmza katika ziara hiyo Mwakilishi wa Ujumbe wa SADC,Genoveva Kilabuka, alisema kuwa ujumbe kutoka SADC umefurahishwa kuona Tanzania inasonga mbele kwenye utekelezaji wa ujenzi wa viwanda kwani ndiyo azma kubwa kwa nchi pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
Lengo kubwa la ziara hiyo ni kujifunza namna ya uzalishaji wa bidhaa kwa kutumia malighafi mbalimbali za ndani ili kuongeza thamani ya malighalifi hizo kwa kuchakata na kuzalisha bidhaa zilizobora kwa masoko ya ukanda wa Kusini mwa afrika hususani katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
“Kwa kweli tumefarijika kuona Tanzania ya Viwanda inasonga mbele sawasawa na mikakati yetu ya kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, huu ni mkakati mkubwa wa nchi na SADC ambao unasisitiza ujenzi wa viwanda ili kutengeneza ajira kwa vijana wengi, kwa hiyo tumeendana kabisa na kauli mbiu ya mwaka huu ya Wiki ya viwanda SADC, “ kwa hiyo viwanda hivi ni moja ya alama kubwa Nchini kwetu”, Alisema Genoveva.
Alisema kuwa katika kutekeleza mikakati ya kufanya viwanda kuwa endelevu Jumuiya ya SADC ni muhimu kwa soko la bidhaa zinazozalishwa nchini, SADC inajikita zaidi kusisitiza ujenzi wa Viwanda na ikiwa Wilaya ya Bagamoyo ina takribani viwanda 65 vikiwemo viwanda vikubwa vilivyotembelewa na wajumbe kutoka SADC, viwanda hivyo ni Elven Agri, SAYONA na kiwanda kikubwa Afrika Mashariki na Kati cha kuzalisha Malumalu cha KEDA, na mkakati huo unalenga zaidi kuzalisha ajira kwa vijana wa nchi wanachama SADC.
Genoveva alitoa rai kwa wazalishaji wa viwanda nchini kuchangamkia Fursa zilizoko SADC ili kuweza kupanua masoko kwa bidhaa zao kwenye nchi mbalimbali zilizoko Ukanda huo wa Afrika, kwani shughuli za Jumuiya hiyo sasa zitahamia Tanzania ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa SADC kwa muda wa mwaka mmoja.
“Ni rai kwa wenye viwanda kama hiki cha KEDA kinachotoa ajira za moja kwa moja kwa watanzania 1,000, na ajira ambazo siyo za moja kwa moja 3,000, tumieni fursa hii ambayo Tanzania tutakuwa wenyeji wa Jumuiya ya SADC kwa muda wa Mwaka mmoja ili kujitangaza na kupata soko, kwani shughuli nyingi za Jumuiya hii zitafanyika Tanzania”, Alisisitiza Genoveva.
Kwa Upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Bagamoyo, Kasrida Mgeni kuwa ni fursa kubwa kutembelewa na Ujumbe wa SADC kwani ujio wao utafungua mtandao mkubwa wa kujua masoko ya kupeleka bidhaa zao kwenye nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ya kusini mwa Afrika.
Mgeni alisema kuwa kati ya mikoa ambayo ina viwanda vingi, Mkoa wa Pwani moja wapo huko halmashauri ya Bagamoyo ikiwa na viwanda takribani 65 huku viwanda 6 vikiwa ni vikubwa na ugeni huo ulipata kutembelea viwanda vitatu vikiwemo Elven Agri, SAYONA na kiwanda cha kuzalisha Malumalu cha KEDA.
“Ujumbe huu ni muhimu sana kwetu, na kama mnavyofahamu Mkoa wetu wa pwani una viwanda vingi na Wilaya yetu ya Bagamoyo tuna takribani viwanda 65,na viwanda 6 kati ya hivyo ni vikubwa kwa hiyo ugeni huu utaweza kufungua Fursa ya kupata masoko kwa Nchi wanachama wa SADC”, Alisema Mgeni.
Mgeni alisema kuwa wawakilishi hao kutoka SADC, wataiwezesha Serikali, Wananchi pamoja na wawekezaji kupat fursa kubwa ya masoko na kutengeneza faida kubwa itakayowezesha ujenzi wa viwanda vingine na kutengeneza ajira kwa vijana nchini.
Naye Afisa Masoko kutoka kiwanda cha Alven Agri, Salumu Kabuluta alisema kuwa ugeni wa SADC katika kiwanda hicho siyo tu fursa kwa nchi bali utawezesha uzalishaji kuimarika na kuweza kutimiza kikamilifu ujenzi wa Tanzania ya Viwanda kama Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza kuwa na uchumi wa viwanda.
“Tukiendana na sera ya Serikali ambayo inataka Tanzania iwe na viwanda vingi na tukihusianisha na hii wiki ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC, sisi kama kampuni ya kitanzania tuahakikisha zaidi suala la viwanda linafanikiwa na sasa nchi yetu inaenda kuwa wenyeji wa SADC kwa hiyo masoko ambayo yapo kwenye nchi hizi 15 tutaweza kuyafikia kwa kirahisi.
Alisema kuwa mpaka sasa bidhaa zao zimefika nchi hizo zikiwemo Zambia, Congo DRC, Malawi na Botswana na Mkutano wa SADC itakuwa ni kichocheo zaidi ya Bidhaa zao kuweza kuenda kwenye nchi hizo 15 ili kukuza masoko ambayo hapo awali hayakuwepo.