Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hadi sasa takribani madereva 102 wamekumbana na adhabu ya kudeki kipande cha kilomita 1 ya barabara kwa makosa mbalimbali.
Amesema kampeni hiyo imezaa matunda tangu alivyoagiza kwa Askari wa Usalama Barabarani kuwa wasiwapige faini madereva wa magari watakaotupa uchafu hovyo na badala yake wawape kipande cha Km 1 cha barabara apige deki.
Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kusisitiza kampeni yake ya usafi kwa wakazi wa Dar es Salaam, ambapo amesema suluhu ya kukomesha madereva wa magari binafsi si kuwapa faini bali ni kuwapa adhabu ambayo itamuumiza na kumfanya asirudie kosa hilo tena.
''Si dhambi ukikamatwa Mwenge au Ubungo ukaenda kupiga deki Mbagala, tutaangalia tu barabara iko wapi tuone, utatusaidia kusafisha barabara zetu ili ziondoe kabisa vumbi ile barabara mpya izidi kuonekana mpya'', amesema Makonda.
Makonda amesema kwamba, kuanzia Jumatatu ya Agosti 5, Serikali ya mkoa huo itaongeza askari wengine takribani 500 kwa ajili ya kuhimiza usafi, ikiwa ni kampeni yenye mlengo wa kuhimiza usafi kwa jiji hilo ambalo kwa sasa linajiandaa na ugeni mkubwa wa viongozi takribani 16 wa SADC.