Ukweli usemwe:Wanaume wanaposhindwa kuwajibika katika malezi, iweje lawama zielekezwe kwa wanawake?



Malezi bora na timamu, yanapaswa kuwashirikisha wazazi wote wawili, yaani baba na mama. Wazazi hawa wanaposhirikiana katika kuwapa watoto wao malezi yenye taratibu njema za kimaadili, ni dhahiri kabisa kuwa, watakua na kuwa watu wazima wa kutegemewa na ambao watakuwa ni kielelezo cha kuigwa kwenye jamii yetu.

Lakini katika hali halisi, akina mama peke yao ndiyo wamekuwa wakiachiwa mzigo na majukumu yote ya kuwatunza na kuwalea watoto wao bila ushiriki wa kina baba. Na mara nyingi watoto hawa wanapogeuka na kuwa waasi na watukutu, lawama zote huwaendea akina mama. Ni jambo linaloudhi na kukatisha tamaa, tunapowaona akina baba wengi wakishindwa kuchukua na kuubeba wajibu wao kama ‘baba’ na viongozi wa familia ambao, watoto wao wanapswa kuiga mfano kutoka kwao.

Kwa kawaida, mtoto anakuwa ni jukumu la mama, hadi akiharibika au akinyookewa. Kama akinyookewa, baba hujifanya kwamba, yeye ndiye aliyehusika kumfanya mtoto awe hivyo, wakati hakuwa akijua alikuwa akisoma darasa la ngapi. Mtoto anapoharibika, baba huruka hatua nyingi akimlaumu mama kwamba, alimdekeza mtoto. Akina baba wengi wanaona kuwa, wajibu wa kuwatunza na kuwalea watoto wao, ni wa wake zao peke yao. Wao wanaona kwamba, wanao wajibu wa kutoa amri na kulaumu kuhusu malezi. Ni kama vile wao hawahusiki na watoto wao.

Hali hii ya kutojitambua na kutokubali kufanya marekebisho katika njia ya kufikiri na kutenda mambo na hasa yale yanayohusiana na watoto na familia kwa ujumla kwa upande wa wanaume walio wengi, imekuwa ikisababisha dhuluma dhidi ya wanawake wengi. Akina mama wengi pamoja na kukabiliwa na majukumu mengine ya uzalishaji mali, pia wamekuwa wakibebeshwa jukumu hili kubwa na zito la kuwatunza na kuwalea watoto wao, bila usaidizi kutoka kwa wanaume zao.

Jamii kwa upande mwingine imekuwa ikiwalaumu moja kwa moja akina mama kuwa, wamekuwa wakizembea na kuwadekeza watoto wao na kusahau kwamba, baba wa watoto hao wapo, lakini jamii haitaki kuwagusa wala kuwakemea……
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad