Unaambiwa Wema Sepetu Akiongeza Fyuzi Moja tu ya Shilole Kichwani Ametoboa
0
August 01, 2019
UKITAKA kujua nguvu ya Madam, Wema Sepetu weka bando lako la kutosha kwenye simu yako janja, chukua picha ya mrembo huyo aliyetwaa Taji la Miss Tanzania 2006 halafu sindikiza na ujumbe wa kumsema vibaya uone balaa lake! Wema anapendwa bwana na bahati nzuri yeye mwenyewe anajua kwamba ana nyota ya kupendwa. Mara kadhaa ameshazungumza hilo pindi anapopewa nafasi ya kufanya hivyo na vyombo vya habari. Kupendwa kwake na watu ni fursa tosha.
Ushawishi alionao anaweza kutangaza jambo lake, wanaompenda wakimuunga mkono kwake ni utajiri. Mathalan anaweza kuandaa tamasha kubwa na kuingiza mapato mengi kupitia kiingilio cha mlangoni. Ukimtazama Wema kwa umaarufu wake lazima ujiulize anakwama wapi? Jina kubwa analo, rasilimali watu kwa maana ya ‘koneksheni’ anazo za kutosha lakini kwa nini hatoboi? Hapo ndipo kwenye msingi wa hoja yangu kwamba kuna kitu kimoja tu (fyuzi) anatakiwa kuwa nacho si kingine bali ni ‘akili ya ushindi’.
Zuwena Mohamed ‘Shilole’ hajawahi kugusa anga za Wema kwa maana ya umaarufu tangu anaanza kuigiza hadi alipobadili gia na kufanya muziki wa Bongo Fleva. Jina lake linapaa juu lakini ni levo ile ya kawaida tu lakini kichwani mwake kuna akili ya ushindi.
Siku zote mtu mwenye akili ya kusaka ushindi huwa anaangalia njia za kupita. Shilole ameshajaribu mambo mengi sana katika maisha yake, alishawahi kufungua saluni baadaye akafungua duka la nguo hadi sasa ameingia kwenye biashara ya chakula. Kwenye biashara ya chakula kumemlipa. Kwenye biashara ya chakula amekusimamia vizuri na kumfanya azidi kuboresha kutoka kwenye mgahawa mdogo hadi kuwa nao mkubwa. Ametumia uwanja wa mashabiki wake (Milioni 4.5) katika ukurasa wake wa Instagram kuwavuta wateja.
Hii ni akili ambayo Wema akijiongeza kidogo tu anatoboa maana ana wafausi Milioni 5.4, ni dhahiri kwamba akiwatumia vizuri wanaweza kumpa faida kubwa. Wabadilishe hao watu milioni 5.4 kuwa hela. Inawezekana kabisa hao watu kuwa utajiri mkubwa kwako.
Wema unapaswa kuwa na msimamo katika mambo anayoyafanya. Kutofanya vitu kwa muda kisha kuviacha. Kama una biashara, isimamie hadi ikupe matokeo. Usiwe mwepesi wa kukata tamaa na kuanzisha biashara mpya kila wakati.
Isimamie, ulifungua duka basi hakikisha kweli linafanikiwa. Usiishie njiani, ulishawahi kuzungumza kwamba una moyo wa kusaidia sana marafiki na mwisho wa siku wakakuangusha basi safari hii usiruhusu hilo litokee. Kuwa na akili sasa ya ushindi, wekeza! Fungua miradi na uisimamie kikamilifu. Jijenge sasa kimaisha, jenga nyumba na usiwe tena mtu wa kuishi kwa kupanga. Mtazame Shilole amefanikiwa hilo na sasa anaishi kwake, amedunduliza lakini ameweza wewe ushindwe kwa nini?
Tumia tu kidogo fyuzi ya ushindi ya Shilole. Kuwa mwanamke shupavu, mwenye kuthubutu na kusimamia kile unachokiamini. Usichezee fedha hovyo, wekeza na mwisho wa siku maisha kwako yatakuwa rahisi. Sisi mashabiki wako tunataka kuona ustaa wako unaendana na mafanikio yako, kila lakheri Madam!
GPL
Tags