Ushahidi wa video kesi ya vigogo wa Chadema watumika rasmi mahakamani
0
August 20, 2019
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeangalia rasmi video iliyowasilishwa mahakamani na shahidi wa sita kama kilelezo cha ushahidi katika kesi inayowakabili viongozi tisa wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Kesi inayowakabili viongozi hao wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa ni ya uchochezi.
Mbowe na vigogo wengine wanane wa Chadema walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 27, 2018 wakikabiliwa na mashtaka manane.
Mbali na Mbowe, viongozi wengine walioshtakiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu bara, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.
Wengine ni Ester Matiko mbunge wa Tarime Mjini, Halima Mdee mbunge wa jimbo la Kawe, Ester Bulaya mbunge wa Bunda Mjini, John Heche mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa mbunge wa Iringa Mjini.
Kabla ya kufikishwa mahakamani vigogo hao walikuwa wakihojiwa polisi mara kadhaa toka Februari 2018 ulipofanyika uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni baada ya kudaiwa kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali, ambayo yalitawanywa na polisi
Tags