Klabu ya Liverpool imetamba kwenye tuzo za wanasoka bora wa Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) usiku wa kuamkia leo jijini Monaco, Ufaransa huku beki wake, Virgil Van Dijk akiwaangusha Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Beki Mholanzi, Van Dijk amewashinda Messi na Ronaldo katika tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka barani Ulaya baada ya kutoa mchango mkubwa kwa Liverpool kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mwezi Juni jijini Madrid.
Van Dijk anachukua tuzo hiyo kutoka kwa Luka Modric wa Croatia na kiungo wa klabu ya Real Madrid ya Hispania, ambaye naye aliichukua kutoka kwa Cristiano Ronaldo aliyekaa nayo kwa muda wa miaka miwili mfululizo akiwa Santiago Bernabeu.
Naye kipa namba moja wa Liverpool, Allison ameshinda tuzo ya mlinda mlango bora wa msimu wa 2018-19 wa UEFA, kufuatia mafanikio yake msimu uliopita Anfield.
Aidha, kiungo Mholanzi, Frenkie de Jong ameshinda tuzo ya kiungo bora baada ya kuiwezesha Ajax kufika nusu fainali ya msimu uliopita.
Nyota wa Barcelona, Lionel Messi amefanikiwa kupata tuzo ya mshambuliaji bora wa UEFA baada ya kufunga mabao 12 katika mechi 10 za msimu uliopita.
Naye nyota wa England na Lyon, Lucy Bronze akafanikiwa kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kike wa UEFA.