Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamini Sitta, amewataka vijana wilayani kwake kuhakikisha wanachangamkia fursa zinazojitokeza ikiwemo ya kujiunga na chuo cha ufundi kutokana na vijana wengi hivi sasa kuwa na ndoto za kuwa madereva bodaboda.
Meya Sitta ameyabainisha hayo mara baada ya kukabidhiwa Chuo cha Ufundi kitakachokuwa kinamilikiwa na manispaa hiyo ili kuweza kuwasaidia vijana wengi kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa.
''Kuna vijana wako vijiweni huko wanalalamika vyuma vimekaza, sasa waje chuoni huku waje wachomelee vyuma hivyo wapate ajira, tuwape hela, tuwape na maeneo, vyuma tena haviwezi kukaza hapo'', amesema Sitta.
Aidha Sitta amesema kuwa vijana watakaojitokeza kusoma katika chuo hicho mara baada ya kuhitimu, Manispaa itawatengea eneo maalumu kwa ajili ya kuendeleza ujuzi wao ikiwemo maeneo ya kufungua gereji.