Wakazi wa Mtaa wa Kilimahewa, Manispaa ya Mpanda, walikumbwa na taharuki baada ya kuvamiwa na nyati na kulazimika kujifungia ndani ya nyumba zao.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Cristophar Masumo, alisema tukio hilo lilionekana kuwapa mshtuko wananchi, huku wanafunzi wakishindwa kwenda shule.
Alisema tukio hilo lilitokea jana saa 2 asubuhi Mtaa wa Kilimahewa jirani na Shule ya Sekondari Shanwe.
Mmoja wa wakazi wa mtaa huo, Lina Philemon, alisema alikuwa akiosha vyombo nyumbani kwake, akafuatwa na jirani yake na kumwambia amemwona ng’ombe amelala jirani na nyumba yake.
Alisema kuwa hali hiyo ilimfanya atoke nje kwenda kutazama, lakini akiwa bado anashangaa, jirani mwingine alipiga yowe na kumwambia akimbie atakufa kwa sababu huyo si ng’ombe.
“Nililazimika kurudi ndani ya nyumba yangu na kujifungia ndani na familia yangu tukipiga yowe kuomba msaada,” alisema.
Naye Rose David alisema yeye aliona umati mkubwa wa watu wakikimbia ovyo, huku wakipiga yowe kuomba msaada.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Shanwe, Salaphina Pikilini anayesoma darasa la sita, alisema tukio hilo lilitokea wakati akiwa anakwenda shule na mwenzake, walimwona nyati huyo, lakini hawakutambua kama ni mnyama hatari.
"Wakati tunaulizana na wenzangu, yule mnyama alinyanyuka na kuanza kutufuata upande wetu, tulikimbia kasi kujiokoa,” alisema.
Askari wa Maliasili walifika na kukuta watu wamejifungia ndani ya nyumba zao, huku nyati akiwa anazunguka zunguka eneo hilo.
Walimpiga risasi mbili ambazo hazikumpata vizuri, hadi mkazi wa eneo hilo, Bila Yusuph aliyekuwa na bunduki yake kumpiga risasi tatu zilizompata.
Baada ya kuuawa nyati huyo, wananchi walifurika eneo la tukio wakiwa na mapanga na visu kupata kitoweo .
Kutokana na umati mkubwa, askari wa Maliasili na wale wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walilazimika kuwatawanya, kisha kumchukua nyati hadi ofisi za maliasili ambako waligawana watumishi wa Serikali tu.