Walimu wa madarasa ya awali hadi la tatu kote nchini, wamepigwa marufuku kuingia darasani na viboko kwa kuwa kufanya hivyo ni kuongeza woga kwa wanafunzi na kusababisha utoro.
Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Msingi kutoka Ofisi ya Raisi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Jidamva, alisema hayo akiwa kwenye ziara ya siku moja mkoani Kilimanjaro.
Alisema licha ya sheria kuruhusu wanafunzi kuchapwa voboko, utafiti unaonyesha kuwa mwalimu anapoingia darasani na kiboko, humtia mwanafunzi uoga na kusababishia wanafunzi wengi wa madarasa ya awali hadi la tatu kuchukia shule na kuacha.
"Watoto hao ni wadogo na wana uwezo wa kuonyeka bila kutumia fimbo. Naagiza walimu wote kuacha kutumia fimbo wanapoingia madarasani na badala yake kuwatengenezea wanafunzi mazingira rafiki ili kuwawezesha kuipenda elimu na kufanya vizuri katika masomo yao,” alisema.
Alisema mbali na kutoingia na viboko madarasani, pia walimu wakuu katika shule za msingi kuhakikisha madarasa ya awali hadi la saba yanaongea vyema ili kuleta mabadilikio ya kimaarifa kwa wanafunzi nchini.
"Tumepata mradi katika mikoa ya Mwanza na Kilimanjaro, ambapo ulituwezesha kuwasaidia wanafunzi wa madarasa ya awali lakini mradi huo kwa sasa umeondoka na katika ziara yangu ya siku moja mkoani Kilimanjaro naona walimu wameweza kuuendeleza licha ya mradi huo kumaliza muda wake" alisema.
"Madarasa ya awali yanaongea, sasa nataka maofisa elimu mkoa wa Mwanza na Kilimanjaro hakikisheni mnakuwa walimu kwa mikoa mingine ambayo haikupata mradi huu ili kuhakikisha Tanzania nzima madarasa ya awali hadi la tatu yanaongea kupitia rasilimali zinazotuzunguka."
Katika ziara hiyo, Jidamva alitembelea shule za msingi za Kifumbu na Rau kuona juhudi za uboreshaji wa madarasa ya awali kabla ya kusambazwa nchini kote.