Wanaume Wenye Mkono wa Kupiga, Hii Inawahusu..!!!!
0
August 28, 2019
KUNA baadhi ya wanaume au makabila fulani huwa wanaamini bila mwanamke kupigwa, mambo hayaendi. Wengine wanaenda mbali na kusema kupiga ndiyo tamu ya penzi lenyewe. Ili mwanamke ajisikie vizuri, lazima apigwe kidogo na mumewe ili penzi liende sawa.
Wapo wanawake ambao nao wanafurahia. Wanajisikia vizuri kuona wamepigwa. Wakikaa muda mrefu bila ya kudundwa kidogo, wanaona kuna kitu kimepungua. Wanaanzisha chokochoko ya aina yoyote ili waweze kupewa kipigo.
Mke akiwa ana muda mrefu hajapata kipigo, anakuwa kama anaumwa. Mazungumzo yake utayagundua tu, akiwa na mumewe. Anamchokoza ilimradi tu. Akipigwa, baadaye atabembelezwa, atasamehe na maisha yanaendelea.
Na hii niseme, wale wenye tabia hii ni rahisi sana kuwajua. Huwa wanajaribu kuvimbisha. Wanajaribu kutunisha misuli ili kuona wanaume wao watafanya nini huku wakijua kitakachotokea.
Anamjibu mumewe anavyotaka. Kama hiyo haitoshi, anajaribu kumshinikiza ajaribu kumpiga ‘kama yeye ni mwanaume kweli’. Kauli hiyo huwa inachochea moto sana kwa wanaume. Mwanaume huwa anajitathmini, anajiuliza mara mbilimbili kwamba ‘sijakamilika au vipi.’
Anajiamini yeye ni mwanaume, tena rijali ambaye anajua vizuri kumshughulikia mkewe iweje mke ahoji uhalali wa uanaume wake? Jibu la haraka hapo huwa linakuwa kumuonesha huo uanaume wake kwa kumtandika angalau kofi moja.
Baada ya kofi hilo mara nyingi huwa linakuwa ni la utangulizi. Anapima kama atajibu tena ili amuongezee dozi. Akijibu anamuongeza zaidi, baada ya hapo inakuwa ni kipigo cha hasira na madhara yake yanaweza kuwa makubwa zaidi.
Kawaida ya wanaume huwa hawapendi kudharauliwa. Huwa hawapendi kuonekana wadhaifu. Hakuna kitu ambacho kinaweza kumkasirisha kwa kiwango cha juu mwanaume kama kuhoji au kuutilia shaka uanaume wake.
Anajisikia vibaya. Hakubali. Kinachofuata baada ya kuambiwa hivyo huwa ni kuutetea uanaume wake. Kuonesha kwamba yeye si dhaifu na baada ya hapo moyo wake unakuwa umetulia kwatu.
Ukiwahoji wanaume wengi kabla hawajafanya
tukio hilo, wengi wao watakuambia ni tukio baya, hawalipendi hata kidogo. Mara nyingi huwa linatokea ghafla na bahati mbaya kulingana na mazingira. Utasikia sikupanga kumpiga na wala haikuwa dhamira yangu ila basi tu, imetokea!
Amechochewa na maneno ya mkewe. Amekasirishwa na kudharauriwa. Kukejeliwa au kuhojiwa uanaume wake. Hasira inapanda, anapiga!
SOMO KWA WANAWAKE
Ni vyema kuwa makini. Kuepuka kuleta uchochezi kwa mwenzi wako. Hata kama amekukosea, tumia lugha rafiki kumuelewesha kuliko kuonesha dalili za dharau. Kuhoji uhalali wa uanaume wake, kumuonesha kwamba na wewe ni mwamba.
Kwamba unajimudu, unaweza kujibu mashambulizi hata kama kweli unaweza, jifanye tu hauwezi.
KAULI ZENYE HEKIMA
Mwanamke unapaswa kuzungumza na mumeo kwa staha. Tumia hekima, busara na unyenyekevu. Unamuonesha ubabe mumeo ili iweje? Unabishana naye kwa lugha za ukali unategemea nini? Kuna sababu gani wewe kujifanya mbabe mbele ya mumeo?
Anaweza kunyamaza, akakuacha na kuondoka zake je utashangilia ushindi wa kumdhibiti mumeo? Halafu ukisha kuwa mshindi, itakusaidia nini? Mwanamke jishushe kwa mumeo maana kwa namna nyingine ni mpango wa Mungu.
Unaposema mwanaume ni kichwa cha familia, isiishie kwenye kuleta matumizi, kulipia ada watoto na mahitaji mengine bali umpe heshima yake kama kichwa cha familia na kamwe hamuwezi kugombana. Mtaishi vizuri.
KWA WANAUME
Ukishaona mwanamke hakuheshimu, mara kwa mara anapenda kuhoji uhalali wa uanaume wako hakuna sababu ya kumpiga. Mfanye akuheshimu kwa njia ya mazungumzo. Muoneshe kwamba wewe ni mwanaume kweli kwa njia ya mazungumzo.
Epuka kumpiga. Ikiwezekana, ukiona anakujibu, anakupandisha munkari, kwanza jua tu ni haiba ya kike. Si kwamba anaweza kujibu mashambulizi pindi utakaponyanyua mkono kumpiga. Yeye huwa anakujibu tu halafu ukianza kumdunda, anainama kusikilizia kipigo.
MADHARA YAKE
Unaweza ukampiga sehemu mbaya, ukampoteza kabisa. Utapata kesi, ukishampoteza ni suala lingine. Kesi ya Jamhuri itakuwa inakuhusu.
Kama unaona kuna jambo linakukwaza, muache. Tafuta muda mzuri, zungumza naye kwa kutumia lugha rafiki na hakika atakuelewa.
LISIMAMIENI MAPEMA
Ni vyema wote wawili mkachunguzana mapema kabla uhusiano haujakua. Mkafundishana mapema kabla tatizo halijawa kubwa. Mkiona mnashindwana kurekebishana katika lugha rafiki ni vyema mkasitisha safari ili msije kupata kazi kubwa huko muendako!
Tags