Wamiliki wa Blogu, Majukwaa mtandaoni (online forums), Radio na Televisheni za mtandaoni wamepewa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha wote wanasajili huduma hizo kama sheria inavyotaka.
Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo, ametoa muda huo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye manyesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Mihayo amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 4 ya Maudhui ya Mtandaoni ya Mwaka 2018 (The Electronic Postal Communications (online content) Regulations, 2018) wamiliki wa forumu hizo wanatakiwa kuzisajili kama inavyotakiwa na wakikaidi sheria itachukua mkondo wake.
Aidha amewataka wamiliki ambao bado wapo na wanaendelea kutoa huduma hizo, kuhakikisha wanatekeleza sheria hiyo ndani ya mwezi mmoja na endapo watakaidi hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
"Bado wapo wamiliki wa Blogu, Majukwaa mtandaoni (online forums), Radio na Televisheni za mtandaoni wanaoendelea kutoa huduma bila ya kusajili, mamlaka inawataka ndani ya mwezi mmoja kuhakikisha wanasajili kama inavyotakiwa,” amesema Mihayo