Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa onyo kali kwa vyama vya siasa nchini ambavyo vimetangaza kufanya mikutano ya hadhara kabla ya muda uliopangwa kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini.
Waziri Lugola ameyasema hayo wakati alipokuwa katika mahojiano maalum na chombo kimoja cha Habari jijini Dar es Salaam, leo, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi lipo imara kipindi hiki tunapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani, hivyo vyama vya siasa vilivyotangaza kuanza kufanya mikutano ya hadhara kabla ya muda Jeshi lake litavishughulikia ipasavyo.
“Hii naomba eleweka na pia iwekwe akilini, mikutano ya hadhara bado haijaruhusiwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ni kosa kufanya mikutano ya hadhara kabla ya tarehe ya kufanya mikutano ya hadhara pamoja na kampeni haijatangazwa, jana kuna chama kimetangaza kuanza kufanya mkutano wa hadhara, sasa waendelee na mipango yao, alafu tuone nini kitawatokea,” alisema Lugola.
Waziri Lugola alisema Serikali haiwezi kuchezewa na kamwe wanaotaka kuichezea watashughulikiwa pamoja na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Kama wanataka kutikisa kiberiti cha Rais Magufuli watakikuta kimejaa, wasithubutu kuichezea Serikali ya awamu hii, tupo imara na pia tutahakikisha tunalinda amani ya nchi hii kwa nguvu zote, na amani hii tuliyonayo hatuwezi kuipoteza kamwe,” alisema Lugola na kuongeza kuwa;
“Nimekabidhiwa lindo hili na Rais Magufuli ili niweze kulilinda ipasavyo, hivyo basi, wanasiasa wasibiri muda wa kuanza kampeni, na sio kukurupa kufanya mikutano ya hadhara bila ya kufuata taratibu, hilo halikubaliki hata kidogo.”
Pia Waziri Lugola, alipoulizwa kuhusu vituo vya polisi kutotoa dhamana saa 24 kama alivyoelekeza kwa nchi nzima, alishangazwa kama kuna baadhi ya vituo hivyo kuendelea kuvunja maagizo yake, hivyo amewataka wananchi wampigie simu kwa mwananchi yeyote atakaye onewa na askari au mtu yeyote aliyopo ndani ya Wizara na Taasisi zake anazoziongoza.
“Mwananchi yeyote atakayenyimwa dhamana, au atakaye onewa, akikisheni mnanipigia simu, na pia kuna njia nyingi za kutupa hapa Wizarani kupitia mitandao yetu ya kijamii, tovuti pamoja na makamanda mbalimbali walipo katika mikoa yote nchini,” alisema Lugola.
Aidha, Waziri Lugola amepiga marufuku tabia ya Watanzania kuchukua sheria mkononi katika matukio yoyote yanayotokea nchini, alisema kumvamia mharifu na kumpiga ni kosa kisheria pamoja na matukio mengineyo.