Yametimia, Harmonize Mpya Nje ya WCB Usipime...Hela Zipo



DAR ES SALAAM: MAMBO ni moto! Hakuna siri tena juu ya tetesi zilizogeuka habari hot Bongo, juu ya staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kujitoa katika familia ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB).  Baada ya kuzua mjadala wa muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuondoka au kubaki Wasafi, sasa imethibitika bila shaka, Harmonize amechukua kila kilicho chake kwenye ngome ya WCB.


YAMETIMIA

Global Publishers kupitia magazeti yake pendwa, ndiyo ilikuwa ya kwanza kuandika habari kuhusu viashiria mbalimbali vya Harmonize kufungasha virago vyake WCB. Miongoni mwa magazeti yaliyopata kuandika habari zinazohusiana na Harmonize kumwaga manyanga kwenye lebo hiyo ni Ijumaa, Risasi Mchanganyiko na gazeti hili la Risasi Jumamosi.


Katika gazeti la Ijumaa la Julai 26, 2019, liliandika HARMONIZE KUJITOA WASAFI, GIZA NENE, likisindikiza na maneno, Ijumaa lamfungia kazi, mwenyewe afunguka. Gazeti la Risasi Mchanganyiko la Julai 31, 2019 lilikwenda mbele  zaidi na kuandika habari kubwa ukurasa wa mbele yenye kichwa; MENEJA WA HARMONIZE APASUA JIPU, aongea na Risasi, aongea mazito usiyoyajua.

Gazeti hili toleo la Agosti 10, 2019 lilikuwa na habari kubwa yenye kichwa, ISHARA TANO HARMONIZE KUJITOA WASAFI, aanzisha rasmi studio yake, shoo zake za nje usizipimie!


NYOTANYOTA

Katika peukua pekua za timu yetu, uongozi wa WCB na meneja wa Harmonize anayejulikana kwa jina la Mjerumani, wote walikuwa na majibu yenye chenga kuhusu ukweli wa msanii huyo kujitoa WCB.

Majibu yao hayo yaliendelea kuacha ukungu kuhusu ukweli wa msanii huyo kuachia ngazi kwenye lebo hiyo inayomilikiwa na staa daraja la kwanza kwenye Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’. Katika sakata hilo, Diamond alipata kusema: “Kama Harmonize anataka kuondoka aondoke.” Hata mmoja wa mameneja wa WCB, Said Fella ‘Mkubwa’ alipotakiwa kuzungumzia hilo, alisema: “Kama akiamua kuondoka hakuna wa kumzuia.”

Kauli hizo ukichanganya na hatua za Harmonize kuamua kuanzisha rasmi studio yake ya Konde Gang, kumchukua legendari kwenye Bongo Fleva, Shabani Katwila ‘Q Chillah’, kutoonekana kwenye uzinduzi wa Tamasha la Wasafi, lililofanyika Julai 19, 2019 kwenye Viwanja vya Zimbihile mjini Muleba, kuliweka picha wazi kuwa msanii huyo alishaamua kufuata njia yake.


JIPU PWAA!

Lakini juzi, meneja mwingine wa WCB Sallam Shariff ‘SK’ aliweka maelezo kwenye ukurasa wa Instagram wa Wasafi TV, ambayo kwa tafsiri hayana shaka kuwa Harmonize ameondoka na wao kama uongozi wameridhia jambo hilo.

Sallam SK aliandika: “Harmonize ndani ya moyo wake hayupo WCB, lakini kimkataba bado yupo WCB. Ameshaandika barua ya kuvunja mkataba na WCB na kufuata taratibu zote za kisheria na sisi tumempa baraka zote.” Kwa maelezo hayo, hayana shaka kuwa Harmonize ameonyesha nia ya kuondoka na amekubaliwa, kinachosubiriwa ni mambo ya kisheria pekee.


HARMONIZE MPYA USIPIME

Risasi Jumamosi lilipata ushirikiano kutoka kwa mtu wa karibu na Harmonize, ambaye alisema uongozi mpya wa msanii huyo umejipanga kumpaisha zaidi kimafanikio. Akizungumza na Risasi Jumamosi kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mtu huyo alisema: “Harmonize mpya ni hatari. Naweza kusema ni samaki mkubwa alikuwa amewekwa kwenye bwawa, sasa amehamishiwa baharini.”

Anaongeza: “Meneja wake mpya Jembe ni Jembe (Sebastian Ndege) amepanga makubwa sana. Unaambiwa kwa sasa tayari ratiba zake za shoo za nje zimejaa kwa mwaka wote huu, hivi ninavyoongea na wewe amekwenda Uingereza kwenye shoo.


“Yaani kikubwa wameona wamsaidie Harmonize kupaa zaidi kimataifa kwa sababu kwa hapa nyumbani tayari jina lake ni kubwa. Yupo kwenye listi ya mastaa wakubwa kabisa wa juu kwenye Bongo Fleva.

“Siyo kama hatapiga shoo za hapa Bongo, hapana ila wamejipanga zaidi kumtangaza nje ili muziki wake uzidi kujulikana duniani.” Jembe ni Jembe ni mdau wa burudani wa muda mrefu ambaye alianzia Radio Clouds FM ya jijini Dar es Salaam, ambaye kwa sasa anamiliki redio moja jijini Mwanza na kufanya shughuli zake jijini humo.


KONDE GANG KUZIDI KUPAA

Kuhusu lebo yake ya Konde Gang, chanzo hicho kiliendelea kueleza ipo mipango ya kuwasajili wasanii rasmi kuanza kufanya kazi na Konde Gang. “Kingine kilichoamuliwa ni kuipaisha Konde Gang zaidi, kikubwa ni kuchukua wasanii wenye uwezo na kufanya nao kazi, hilo jukumu limewekwa chini ya mameneja wake,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu tetesi za Q Chillah kuwa ameshasaini rasmi katika lebo hiyo alisema: “Hilo halijawekwa wazi bado, lakini kama unavyojua wapo pamoja na wote wameridhia kufanya kazi pamoja.”

Chanzo hicho hakijaweka wazi kama kufanya huko kazi pamoja kuliporidhiwa kama alivyosema, ni kuingia kwenye Lebo ya Konde Gang au vinginevyo. Harmonize hakupatikana kuzungumzia hayo, kwa maelezo kuwa yupo safarini nje ya nchi. Risasi Jumamosi linaendelea kumtafuta msanii huyo ili aweke mambo zaidi hadharani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad