Baba Yake Manara Afunguka Wanachokosea Yanga
0
September 06, 2019
TANGU Yanga imefanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chake na kutangaza usajili mpya, maneno yamekuwa mengi hasa kutokana na aina ya matokeo wanayoyapata katika michezo mikubwa.
Yanga wamekuwa wakipata matokeo finyu pale wanapokutana na timu ambayo ipo katika levo sawa na kikosi hicho ama wamezidiana. Katika michezo minne ya kimataifa ambayo Yanga wamecheza hivi karibuni, wameshinda mechi mbili na kutoka sare michezo miwili.
Kwa sasa Yanga wanajiandaa na mechi ngumu dhidi ya Zesco United ya Zambia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza kutafuta nafasi ya kutinga kwenye makundi ya michuano hiyo. Kuelekea katika mchezo huo, Spoti Xtra limefanya mahojiano na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Sunday Manara ‘Computer’, ambaye ni baba mzazi wa Ofi sa Habari wa Simba, Haji Manara.
“Kwanza nikuambie tu Yanga hii ya sasa ina kikosi bora na chenye wachezaji wazuri, mabadiliko ambayo yamefanywa na uongozi huu wa sasa yameisaidia sana Yanga, kila mchezaji ambaye amesajiliwa ana kitu chake cha ziada mguuni mwake.
“Wanaosema kuwa Yanga hawana timu nzuri, watakuwa hawaujui mpira na muda ukifi ka watakubaliana na hiki ninachokisema kuwa Yanga ni timu bora, hivyo mashabiki wa Yanga watulie na waiamini timu yao,”anasema.
NINI KINAISUMBUA YANGA KATIKA KUFUNGA MABAO?
“Shida kubwa ambayo mimi binafsi nimeiona ipo katika suala la umaliziaji tu, jambo ambalo nalo siyo tatizo kubwa sana, wachezaji au mwalimu mwenyewe anaweza akalifanyia kazi na kila kitu kikawa sawa.
“Kwa sababu utaona kuanzia nyuma timu inacheza vizuri sana hadi kufi ka eneo la katikati, mipira ikifi ka mbele kwa washambuliaji huonekana kama haina faida kutokana na washambuliaji wenyewe kutokuwa na maelewano na muunganiko sahihi katika kufunga mabao.
KOCHA ZAHERA ALIKOSEA WAPI KWA TATIZO HILO?
“Nafikiri kosa kubwa lilifanyika pale ambapo uongozi na kocha walishindwa kuwaweka wachezaji sehemu moja mapema na wakakaa kwa muda mrefu na kuwatafutia mechi ngumu za kirafi ki.
“Endapo hawa wachezaji wangewekwa kambini mapema, nina uhakika kocha angeshatibu hili tatizo la kutoelewana na kila kitu kingekuwa sawa, lakini kama nilivyotangulia kusema, hilo siyo tatizo kubwa sana, mwalimu anaweza kulifanyia kazi na huko mbele timu ikacheza vizuri na wachezaji wakawa wanafunga mabao mengi.
NINI KIFANYIKE SASA ILI KUONDOA TATIZO HILO?
“Hakuna kingine zaidi ya kumpa mwalimu na wachezaji muda wa kulifanyia kazi hilo suala, kwa sababu bila shaka hata kocha na wachezaji wenyewe wanajua shida yao ipo wapi, hivyo mashabiki na wanachama watulie na wampe muda mwalimu.
UNAUZUNGUMZIAJE MCHEZO WA YANGA NA ZESCO?
“Yanga wanashinda mchezo huo, ngoja nikuambie kitu, timu ya msimu huu tofauti kabisa na ile ya msimu uliopita, Yanga hii ni nzuri zaidi na ina wachezaji bora, kila mchezaji ana uwezo wake binafsi wa kuisaidia timu kupata matokeo chanya.
“Zesco ni timu kubwa na ina wachezaji bora kama ilivyo kwa Yanga, kwa hiyo hawatoweza kupata ushindi, safari hii ni zamu yetu kusonga mbele, hii nawaambia hata mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi ushindi upo wanachotakiwa kufanya ni kwenda uwanjani na kuipa sapoti timu yao.
MWANAO MANARA ANAWATAKA SIMBA KUISHANGALIA ZESCO, UNALIZUNGUMZIAJE HILI?
“Mimi namuambia asijifanye mjuaji sana, kwa sababu mashabiki wa Simba siyo watoto wadogo ambao wanaweza kufuata kila kitu ambacho yeye anakisema, hii ni mechi ya kimataifa, kupata ushindi kwa Yanga ni faida kwa nchi nzima.
“Kwa hiyo yeye asilazimishe kile anachokitaka watu wamsikilize, anatakiwa abaki na msimamo wake na watu wengine awaache waamue wenyewe, kwa sababu hata akisema hivyo mwisho wa siku ataumbuka kwa sababu Yanga lazima ashinde kwenye mchezo huo.
Tags