Imeelezwa kuwa Barafu katika mlima Kilimanjaro imepungua kutoka kilometa za mraba 11 hadi kufikia kilometa za mraba 1.7 kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamesababisha kukosekana kwa unyevu unyevu unaopandisha mvua juu mlimani.
Mhifadhi mkuu wa mlima Kilimanjaro Bi. Anjela Nyaki ameyasema hayo wakati kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Moshi ilipotembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kukutana kujadili njia za kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.
Amesema hatua zimeanza kuchukuliwa za kutunza mazingira kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo kwa kupanda miti kwa kushirikiana na wananchi ambapo tafiti zilizofanywa hivi karibuni zimeonyesha mafanikio ya uoto wa asili ambao ulikuwa umepotea kuanza kurejea tena katika hifadhi hiyo .
Mkuu wawilaya ya Moshi Kippi Warioba ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama anasema kwa pamoja kamati hiyo imekubaliana kushirikina na wahifadhi wa mlima huo kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji.