Yondani, Songo Wavuruga Mipango ya Lwandamina

BEKI mkongwe wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani ametamka kuwa kama safu yao ya ulinzi itacheza kwa kufuata maelekezo na mbinu walizopewa na kocha wao mkuu Mkongomani, Mwinyi Zahera basi wapinzani wao Zesco United wanawapiga kwao.



Kauli hiyo aliitoa mkongwe huyo saa chache kabla ya kupanda ndege juzi Jumanne saa nne asubuhi kuelekea Zambia tayari kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.



Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumamosi hii saa kumi kamili kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa huko kwenye Mji wa Ndola, Zambia.



Yondani alisema kuwa kikubwa hawataki kurudia makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo wa awali uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na uliosababisha kuruhusu bao baada ya kupewa mbinu na maelekezo ya jinsi ya kuzuia na kupunguza mashambulizi golini kwao.

Yondani alisema kuwa wataingia uwanjani katika mchezo huo wakiwa tayari wameshazijua mbinu za Kocha Mkuu wa Zesco, George Lwandamina na kikubwa watakachokifanya ni kuzuia njia watakazozitumia katika kushambulia wapinzani wao ili kuhakikisha hawaruhusu bao ugenini.



“Kwa upande wa kocha tayari amemaliza kazi yake ya kuiandaa timu kwa kila nafasi kuipa majukumu yake, upande wetu mabeki tumepewa mbinu na maelekezo ya jinsi ya kulilinda goli letu pale timu inapokuwa haina mpira.



“Mbinu hizo alizotupa ni zile za mchezo uliopita tuliocheza Uwanja wa Taifa baada ya kuwaona wapinzani wetu jinsi wanavyocheza, pia mbinu na mfumo wanaoutumia.



“Hivyo, hatuna hofu ya mchezo huo kwani tayari kwa upande wetu mabeki tunajua tutumie aina gani ya uchezaji ili kuhakikisha tunawazuia washambulia wa Zesco,” alisema Yondani.



Kwa upande wa beki Ally Mtoni ‘Sonso’ alisema: “Tutakachokifanya kama mabeki katika mchezo huo ni kuzuia njia pekee, hatutakubali kuona washambuliaji wa Zesco wakileta madhara golini kwetu.



“Tayari kocha ameshatupa mbinu na jinsi wa kuwazuia washambuliaji hatari wa Zesco, hivyo Wanayanga watarajie ushindi katika mchezo huu ambao ni muhimu kwetu.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad