Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Kangi Lugola, kufuatilia rufaa za malalamiko walizowahi kuziwasilisha ofisini kwake juu ya zuio la Jeshi la Polisi la kufanya mikutano ya hadhara na kisiasa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, Tumaini Makene
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 28, 2019 na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene wakati akizungumza na EATV &EA Radio Digital, ambapo amesema kuwa wameshangazwa na kauli ya Waziri Lugola aliyoitoa hivi karibuni ya kwamba hajawahi kupokea barua kutoka vyama vya upinzania, kuhusu kuzuiliwa kufanya mikutano yao.
''Kama kweli anataka kutenda haki, afanyie kwanza kazi na maamuzi ya rufaa ambazo ziko mezani kwake kama akibisha, sisi tuko tayari kumpelekea vielelezo vya namna ambavyo madiwani na wabunge wetu ambao wameshapeleka malalamiko ofisini kwake baada ya kuwa wamezuiliwa kufanya mikutano'', amesema Makene.
Waziri Lugola alitoa kauli hiyo Septemba 26 Jijini Dodoma baada ya kuzindua ofisi ya Kituo cha Sheriaa na Haki za Binadamu (LHRC), ambapo alisema kuwa, ''tangu nimeteuliwa sijawahi kupokea hata rufaa kulalamika kuwa wamenyimwa haki, badala yake wanakurupuka na kulalamika sasa mimi nifanyeje'', alisema Lugola.