Daktari Aanika Ugumu wa Mama Diamond Kuzaa Tena
0
September 25, 2019
UJAUZITO anaopata mwanamke mwenye zaidi ya umri wa miaka 50 huja na changamoto nyingi za kiafya na ugumu wa kuzaa, Dk Gofrey Chale wa jijini Dar es Salaam ameliambia Gazeti la Ijumaa Wikienda.
Dk Chale alitoa kauli hiyo wakati akitolea ufafanuzi habari ya mama mzazi wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim almaarufu Bi Sandra au Mama D kudai kuwa ni mjamzito.
MAMBO YALIANZA HIVI
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mama D kupitia ukurasa wake wa Instagram aliweka picha akiwa amevaa gauni na baadaye kumjibu mmoja kati ya mashabiki zake aliyempongeza kuwa amependeza; “Hahaa… Diamond atapata mdogo wake… basi subirieni mdogo wake wa mwisho…”
Maneno hayo yaliaminiwa na wengi kuwa mama huyo wa msanii Diamond au Mondi ni mjamzito na kwamba anatarajiwa kujifungua hivi karibuni kufuatia maneno hayo kuungwa mkono na bintiye, Esma Khan kuwa ana furaha kupata mdogo wake kwani wao wamezaliwa wawili tu.
Kilichofuata baada ya hapo ni mashabiki wakiwemo mastaa wa Bongo Muvi kuendelea kumpongeza kwa ‘hongera’ za kumwaga.
HABARI ZASAMBAA KAMA MOTO WA KIFUU
Kama ujuavyo Waswahili hawana dogo, habari hizo zilianza kuenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa Diamond yuko mbioni kupata mdogo wake kutoka kwa baba yake wa kambo aitwaye Maisara Shamte ‘Anko Shamte’.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Mama D kuvumisha kuwa ni mjamzito baada ya mwaka jana kufanya hivyo na baadaye habari kuripotiwa kuwa ujauzito wake ulichoropoka.
HUYU HAPA DOKTA CHALE
Baada ya suala la ujauzito wa mama huyo wa msanii maarufu nchini kuwa ‘hoti’, Gazeti la Ijumaa Wikienda lilimtafuta daktari wa akina mama, Dk Chale ili azungumzie uwezekano wa Mama D kupata mtoto katika umri huo wa miaka 50.
“Uwezekano wa kuzaa upo, inategemea na afya yake kwa sababu kadiri mwanamke anavyokuwa na umri mkubwa ndivyo afya yake ya uzazi huwa katika changamoto nyingi.
“Ingawa tafiti zinaonesha kuwa ubora wa huduma za afya duniani umepunguza kiwango cha vifo kwa wanawake wanaojifungua kwenye umri mkubwa, lakini tatizo bado lipo.
“Miongoni mwa matatizo ambayo mwanamke mwenye umri wa miaka arobaini hadi arobaini na tano na kuendelea hukutana nayo kipindi cha ujauzito ni kupata kisukari, kupanda kwa shinikizo la damu, kiharusi na matatizo ya moyo. Mambo haya yote ni hatari kwa mama mjamzito wakati wa kujifungua,” alisema Dokta Chale.
RIPOTI ZA UTAFITI
Hata hivyo, tafiti zilizofanywa hivi karibuni na vyuo mbalimbali vya afya duniani zinaonesha idadi ya wanawake wenye umri mkubwa kupata ujauzito na kujifungua imekuwa ikiongezeka.
Ripoti Muhimu ya Takwimu ya Idara ya Afya ya Utah nchini Marekani inaonesha kuwa wanawake 80 wenye umri wa miaka 45 au zaidi walijifungua mnamo 2016, kutoka 62 mwaka 2015 na 70 mwaka 2014.
Naye Dk Cynthia Austin, Mkurugenzi wa Kliniki ya Urutubishaji Mayai ya Invro nchini Marekani anasema;
“Ingawa mishipa ya damu hupoteza ufanisi wake kadiri mwanamke anavyoongezeka umri na kusababisha hatari ya kupata mtoto mwenye uzito mdogo au changamoto za kiafya, lakini hilo si jambo la kuogopesha.
“Endapo mwanamke atavuka kikwazo cha kupata ujauzito kwa njia ya kawaida bila kupandikiza haya mengine yanaweza kuangaliwa na madaktari.”
DK CHALE TENA
Wakati Dk Cynthia anaeleza hayo, Dokta Chale kwa uzoefu wake anaeleza kuwa ujauzito wakati mwingine limekuwa jambo lenye changamoto nyingi, lisilokuwa na uzoefu.
“Zamani ilikuwa mwanamke mwenye umri mkubwa aliyezaa watoto kadhaa ndiyo alionekana ni mzoefu na hakukuwa na shida katika kujifungua.
“Lakini siku hizi kumetokea vitu ambavyo vinawafanya wao waonekane kuwa na hatari zaidi wakati wa kujifungua, ninachoweza kusema afya ya mzazi ndiyo kitu bora kuliko kingine.
“Awe na umri mkubwa au mdogo maadam anakwenda kwenye siku zake na afya yake ni nzuri ndiyo itakayoweza kuamua usalama wake wakati wa kujifungua.”
WATOTO WA MAMA D
Katika maisha yake ya miaka hamsini, Mama D amefanikiwa kupata watoto wawili ambao ni Diamond aliyezaa na Abdul Juma na Esma ambaye alizaa na mwanaume aitwaye Khan.
Hata hivyo, kadiri umri unavyozidi kumtupa mkono Mama D amekuwa akionesha kuwa na kiu ya kupata mtoto mwingine wa tatu na endapo hilo litafanikiwa atakuwa amemzalia chema mume wake wa sasa, Shamte.
Tags