Diwani CUF ahofiwa kutekwa
0
September 01, 2019
Na Ahmad Mmow, Lindi.
Diwani wa kata ya Mirui, halmashauri ya wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Saidi Mmogeliu (CUF) anahofiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Akizungumza na Muungwana Blog kuhusu tukio hilo kutoka Liwale, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mohamed Mtesa (CUF) alisema Mmogeliu alichukuliwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake mtaa wa Mungurumo, mjini Liwale. jana usiku, majira ya saa tano baada ya watu hao kujitambulisha kuwa ni askari wa jeshi la polisi.
Mtesa ambae ni diwani wa kata ya Liwale B, alisema watu hao ambao walikwenda nyumbani kwa Mmogeliu kwa gari, walipiga hodi nakumuomba waondoke nae kwenda kituo cha polisi akatoe maelezo, jambo ambalo diwani huyo alipinga kabla ya watu hao ambao idadi yao inatajwa kuwa sita kutishia kuvunja mlango wa uwa.
'' Nimetoka polisi, nimemkuta mkuu wa kituo amesema hakuna askari yeyote aliyetumwa kumkamata mhemiwa diwani, nimemuacha mkewake anaandikisha maelezo yake hapo kituoni na wameniambia wanafuatilia,'' alisema Mtesa.
Aliendelea kusema kwamba Mmogeliu alikubali kufungua geti na kuondoka na watu hao baada ya kuja jirani yake anayejulikana kwa jina la mama Kichwamba.
''Alimtuma mkewake akamuite mwenyekiti wa kitongoji au jirani kabla hajaondoka ambapo alipokuja jirani huyo watu hao walimuhakikishia atarudi salama baada ya kutoa maelezo kituoni, ndipo walipoondoka nae kwa gari waliyokwenda nayo hapo,'' alisema Mtesa.
Mwenyekiti huyo alisema mke wa Mmogeliu bado alikuwa na mashaka kama mumewe alipelekwa polisi. Kwahiyo alikwenda kwa mwenyekiti wa mtaa huo ambae baada ya kuambiwa hayo aliamua waende polisi kuthibitisha, usiku huo majira ya saa 7.00. Ambako waliambiwa diwani huyo hakuwepo kituoni hapo na hakuna askari waliotumwa kwenda kumkamata diwani huyo( Mmogeliu) maarufu kwa jina la Koffi.
Kamanda wa polisi wa mkoa ( RPC) wa Lindi, kamishna msaidizi wa polisi, Pudensiana Protas alithibitisha kutokea tukio hilo kwa kusema '' Nasisi( Jeshi la polisi) tumepata ya kuwepo jambo hilo. Kwahiyo tunafuatilia ili kujua nini kimejiri. Nikwe tumepokea taarifa na tunafuatilia,'' alieleza na kusisitiza kamanda Pudensiana.
Tags