Hatua itakazochukua Tanzania baada kupata ndege
0
September 05, 2019
Serikali ya Tanzania imesema ipo katika mchakato wa kufungua kesi ya kudai fidia ya pesa iliyotumika kuendeshea kesi ya Ndege ya ATCL, iliyokuwa ikishikiliwa nchini Afrika Kusini.
Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt Damas Ndumbaro, amesema kuwa licha ya wao kushinda kesi dhidi ya kushikiliwa kwa ndege ya ATCL, lakini lazima itachukua hatua stahiki dhidi ya aliyefungua kesi hiyo.
''Sisi tumemaliza kesi kinachofuata ni kudai fidia kwa sababu Mahakama imetupa gharama yote ya kesi, kwahiyo tutadai gharama za kesi na fidia ya hasara ambayo tumeipata kutokana na kesi hii'', amesema Waziri Ndumbaro.
Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 ilizuiliwa nchini Afrika ya Kusini kwenye uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg, kwa amri ya Mahakama, siku ya Agosti 24 na iliachiwa huru Septemba 4, 2019, hii ni baada ya Serikali kutuma jopo la Mawakili kwa ajili ya utetezi wa kesi hiyo.
Hermanus Steyn alifungua kesi ya fidia dhidi ya serikali ya Tanzania kwa kile alichodai kuwa alikuwa anamiliki ardhi, mifugo na mali nyingi ambazo zilitaifishwa na serikali ya Tanzania miaka ya 1980 na ilipofika miaka ya 1990 walikubaliana fidia atakayolipwa, kwa ujumla wake dola milioni 33 na tayari ameshalipwa dola milioni 20 kati ya hizo.
Tags