Hizi Hapa Hatari Tano(5) Anazoweza Kukutana Nazo Mwanao Mtandaoni...

Mara kadhaa kupitia wasaa huu tumezungumza juu ya matumizi ya mtandao na athari zake, chanya na hasi. Leo tunakutanabaishia aina tano kuu za hatari anazoweza kukutana nazo mwanao awapo mitandaoni na namna bora ya kukabiliana nazo ili kupafanya mtandaoni mahali salama kwa mwanao.

Maudhui yasiyofaa. Mtandaoni kuna maudhui chungu nzima kuanzia nyimbo za ibada hata filamu za utupu. Ingawa waandaaji wa maudhui wanaweza kuweka maangalizo juu ya umri wa nani anapaswa kuona nini – mtandao haubagui na mara nyingi hasa hapa kwetu watoto wetu wanatumia ama simu zetu, kompyuta na pengine ‘tablets’ zetu wazazi kuingia mtandaoni. Namna hii wanaweza kuangalia mambo tunayotumiwa na watu wazima wenzetu ama mambo ambayo tumekwisha yafungua wakaendelea ‘kufurahia.’

Kufanya mawasiliano na watu wasiofaa. Mtandaoni wapo marafiki – tunaowafahamu vyema na tusio-wafahamu hata chembe. Sisi wenyewe watu wazima kila uchao tunapokea maombi ya marafiki wapya. Mtoto vilevile awapo mtandaoni hili halikwepi. Wapo watu wasio-waaminifu ambao kutwa wanatafuta watoto wadogo kuwalaghai ama kuwarubuni kupitia picha za ngono ama hata kuwaibia ‘pocket money’ ambayo sisi wazazi tunavuja jasho kuwatimizia. Je unajua utafiti wa hivi karibuni ulionyesha kuwa mtoto mmoja wa kitanzania anao marafiki mpaka zaidi ya 5,000 kwa wastani katika mitandao ya kijamii?

Mitandao inaweza kumuharibia mwanao sifa. Watoto, kama ilivyo sisi watu wazima, wanapenda kuwa maarufu. Umaarufu wa mitandaoni umewafanya watoto wapige picha wakiwa watupu, wakiogelea ama hata wakipata kumbato, mabusu na mambo kama hayo huku wenzao wakiwachukua filamu ama picha. Yote haya hupakiwa katika mitandao ya kijamii kwa minajili ya kupata ‘likes’ na maoni (comments). Bahati mbaya mtandao hausahau. Picha na filamu hizi zitadumu mitandaoni hata watakapohitimu elimu na wakawa ‘watafuta ajira’ ama hata viongozi katika jamii.

Matumizi yalopitiliza hadi kuleta athari za utegemezi wa mtandao. Upo usemi unaoibuka kwa sasa kuwa maisha hayawezekani pasi na mtandao. Hii kwa watoto ina maana kuwa wataathirika kimakuzi, masomoni, kiroho na hata kimahusiano. Itakuwa nadra kwao hata kujenga hoja wanapokuwa na marafiki hata kwetu sie wazazi wao. Marafiki wao takribani wote watakuwa penye ‘screen’ za kompyuta, n.k.

Athari za kibiashara. Upo ushahidi wa mzazi mmoja aliyeikuta picha ya mwanaye aloipakia mtandaoni katika mabango ya matangazo barabarani (billboards) alipokuwa safarini nchi jirani. Makampuni kwa sasa yamehamishia ‘vita’ ya masoko mtandaoni. Kila unapoingia kuperuzi unaulizwa ulipo (location), umri na hata mawasiliano yako binafsi. Yote haya ni mambo ambayo mtoto kamwe hawezi kuyakabili. Mara nyingi atagawa taarifa hizi kama njugu na mwishowe atakuwa ‘soko-mjinga’ la bidhaa lukuki hata zenye kuhitaji matumizi ya watu wazima pekee.

Ufanyeje? Badala ya kumnyima mtoto mtandao mpe mafunzo ya matumizi bora ya mtandao. Wewe ndiye mlinzi nambari moja wa mtoto wako. Mpe nyenzo ili kwazo ajikinge na majahili toka kote duniani mtandaoni. Anza kwa kujifunza wewe namna bora ya kutumia mtandao kwa miongozo chungu nzima inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano hapa kwetu Tanzania.

Vilevile makampuni mengi makubwa mtandaoni sasa yametia saini makubaliano ya kumlinda mtoto mtandaoni. Facebook, YouTube, Google na mengine. Soma sehemu ya vigezo na masharti ya mengi ya makampuni haya ili kuziba mianya ya wewe na mwanao kuingia katika tovuti zisizofaa hasa kama unatumia kifaa chako hicho na mwanao uwapo nyumbani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad