Imethibitika, kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba alifikia makubaliano binafsi na uongozi wa Paris Saint-Germain, lakini mambo yalivurugika siku chache kabla ya dirisha la usajili wa majira kiangazi kufungwa mwanzoni mwa mwezi huu.
Jarida la michezo la Calciomercato la nchini Italia, limefichua siri hiyo iliyokua ikiendelea nyuma ya pazia, na limeeleza Pogba alikubali mshahara wa Pauni 429,000 kwa juma.
Sababu kubwa iliyotajwa hadi kuvurugika kwa dili hilo, ni hatua ya mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar, kushindwa kufanikisha azma yake ya kurejea FC Barcelona
Hata hivyo Jarida hilo limeeleza kuwa, mbali na PSG kupewa nafasi kubwa ya kumsajili Pogba, pia klabu nyingine kama FC Barcelona na Real Madrid zilikua tayari kupambana kwenye kinyang’anyiro cha usajili kiungo huyo.
“Meneja wa PSG Thomas Tuchel, alihitaji huduma ya kiungo huyo, na mara kadhaa aliutaka uongozi wake kufanya jitihada za kufanikisha dili hilo, lakini mambo yalikwenda kombo.” imeelezwa katika taarifa iliyochapishwa kwenye jarida la Calciomercato.
Kwa mantiki hiyo Pogba amekosa dili nono la mshahara wa Pauni milioni 22 kwa mwaka, na huenda ingemuweka katika ramani tofauti, endapo angefanikiwa kurejea nyumbani kwao Ufaransa.
Katika hatua nyingine kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas, nayo imetajwa kuwa sababu ya kumbakisha Pogba Man Utd, kwa maslahi ya kibiashara, japo tayari meneja Ole Gunnar Solskjaer, alionyesha dalili zote za kutaka kumuachia.