Meli ya mafuta iliyokuwa na bendera ya Uingereza na ambayo ilikuwa ikishikiliwa katika bandari ya Abbas nchini Iran kwa zaidi ya miezi miwili, imeanza safari kuelekea Uingereza. Tovuti maalum inayofuatilia safari za baharini imeripoti hayo.
Hapo jana, msemaji wa serikali Ali Rabiei alitangaza kuwa mchakato wa kisheria umekamilika na meli hiyo inayomilikiwa na Sweden iko huru kuondoka.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, tovuti ya Tanker Trackers imeandika kuwa picha za satelaiti zinaonyesha kuwa meli hiyo imeondoka.
Mnamo Julai 19, kikosi maalum cha askari wa mapinduzi nchini Iran kiliizingira meli hiyo kwa jina Stena Impero katika mlango bahari wa Hormuz.
Meli hiyo ilikamatwa kufuatia tuhuma za kushindwa kuitikia wito wa dharura uliotolewa baharini.
Hata hivyo kukamatwa kwa meli hiyo kulitizamwa kama ni kulipiza kisasi baada ya maafisa wa Uingereza kuikamata meli ya Iran mapema mwezi Julai kwa tuhuma za kusafirisha mafuta kupeleka Syria.