Jamali Ameeleza Mahakama Fedha Alizolipwa na TFF Alipewa Kihalali
0
September 02, 2019
Aliyekuwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa fedha alizolipwa na TFF, alilipwa kihalali.
Malinzi alieleza hayo leo wakati akiendelea kutoa utetezi wake katika kesi inayomkabili ya utakatishaji fedha, baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.
Akiongozwa na Wakili wa utetezi Richard Rweyongeza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde , Malinzi alidai kuwa alieleza kuwa dola za Marekani 2400 alizolipwa na TFF ilikuwa ni malipo baada ya kuhudhuria mkutano wa FIFA nchini Mexico, Mei 16, 2016, ambapo wakati anaenda katika mkutano huo alitumia fedha zake mfukoni, hivyo aliporudi nchini alilipwa fedha hizo na TFF.
Vile vile dola za kimarekani 7000 anazodaiwa kujipatia kwa njia udanganyifu, alilipwa alipewa kilahalali na TFF, baada ya kuchukua fedha yake mikononi kulipa Kocha wa timu ya vijana kiasi cha dola 7000.
” TFF walinilipa dola za kimarekani 7000 kwa sababu niliikopesha TFF na kumlipa mshahara kocha wa timu ya taifa ya Serengeti Boys , Kim Paulsen, kipindi hicho TFF haikuwa na fedha ” alidai Malinzi.
Malinzi alidai hata dola za kimarekani 10,000 alizolipwa na TFF, alilipwa kihalali kwa sababu aliikopesha TFF .
Malinzi alidia kuwa dola za kimarekani 10,000 alitoa yeye kutoka mfukoni mwake kwa ajili ya kuilipia timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 walikuwa wanacheza na timu ya vijana ya Misri na hiyo ilikuwa Juni 16, 2016.
” Nilikuwa natoa fedha zangu mfukoni kuwalipita wachezaji alafu baadae fedha zikipatikana TFF inanilipa, hivyo niseme tu fedha hizo nilipewa kihalali na TFF na wala sikujipatia kwa njia ya udanganyifu kama jinsi shtaka la 26 linavyoeleza kuwa nilijipatia fedha hizo njia ya udanganyifu” alidai Malinzi.
Mshtakiwa huyo aliendelea kujitetea kuwa kuanzia mwaka 2014 hadi 2016, ameikopesha TFF kiasi cha Sh 320milioni.
Malinzi alidai akiwa kama sehemu ya familia wa TFF na kama kiongozi alikuwa anaikopesha fedha TFF.
” Katika kipindi changu, walikuwepo watu mbalimbali ambao walikuwa wakiikopesha TFF, lakini mimi ndio raisi wa kwanza wa TFF ambaye nilikamatwa na kufikishwa mahakamani” alidai Malinzi
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Celestine Mwesigwa.
Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wako rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku Flora akiwa nje kwa dhamana.
Tags