Jeshi La Polisi Mkoani Dodoma Lamnasa Mtu Mmoja Akijaribu Kutorosha Madini
0
September 23, 2019
MTU mmoja Khalifa Mohamed Kinyaka (51) anashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani Dodoma, kwa tuhuma za kutorosha na kusafirisha viroba sita vya madini vyenye uzito wa kilogramu 410.75.
Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Gilles Muroto, amesema mtu huyo alikamtwa katika basi la abiria la Jambo Express, lenye namba za usajili T 704 DLF, linalofanya safari zake kati ya Katesh na Dar es salaam.
Amesema mbinu iliyotumiwa na mtuhumiwa ni kupanda basi tofauti na lile alilopakia viroba vingine vitano, katika basi la Emigrace lenye namba za usajili T 730 DGL lililokuwa likiendeshwa na Adrian John Temba (32), likitokea Babati Manyara kuelekea jijini Dar es salaam.
Hata hivyo uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaonesha kuwa madini hayo yametoka katika machimbo ya Kijiji cha Yobo Kwahemu Wilayani Chamwino, na juhudi za kuwapata washiriki na wanunuzi zinaendelea ili kuweza kuwafikisha Mahakamani.
Akifafanua juu ya taratibu husika za usafirishaji madini, Mhandisi Migodi wa Ofisi ya Madini Dodoma Sasi Marwa, amesema muhusika alipaswa kuwa na vibali toka eneo husika na kwamba tathmini itafanywa ili kujua thamani halisi ya madini hayo.
Tukio hili linakuja ikiwa ni muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma, kuwakamata watu zaidi ya 70 kwa makosa mbalimbali Septemba 21 mwa ka huu , ikiwemo usafirishaji wa mafuta ya vyombo vya moto kwa njia hatarishi.
Tags