JPM Awapa Siku zingine 7 Wahujumu Uchumi Kutubu
0
September 30, 2019
RAIS John Magufuli amewaongezea siku saba nyingine watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi wanaosota mahabusu ili wakiri makosa yao na kuzirudisha fedha wanazodaiwa kuzichukua.
Ametoa rai hiyo kutokana na barua zao kukwama kwenye ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), mikoani na kwenye ofisi za magereza.
Magufuli amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 30, 2019, wakati akipokea taarifa ya ushauri alioutoa kwa DPP, siku kadhaa zilizopita akimuomba awasamehe watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi watakaokuwa tayari kukiri na kurudisha fedha hizo ambapo DPP, Biswalo Maganga, alimuomba rais aiongezee ofisi yake siku tatu zaidi kwa ajili ya kuupitia kikamilifu mchakato mzima wa zoezi hilo na kuwapa nafasi watuhumiwa hao na wengine kutubu na kurejesha fedha.
Hojh kubwa alizotoa Rais Magufuli ni:
“DPP, sikutegemea kama watuhumiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi wangeandika barua kuomba wasamehewe. Kiasi cha Tsh bilioni 107.842 kitakuwa kimeokolewa kutokana na hawa waliotubu na wako tayari kulipa. Naomba muwaruhusu walipe kwa awamu kadri mtakavyokuwa mmekubaliana na Serikali.
“Kwa sababu mwanzoni nilitoa siku sita, na DPP umeomba niwaongeze siku tatu kutokana na barua za watuhumiwa kukwama mikoani, kwenye magereza au hazijafika kwako, ninawaongeza siku nyingine saba ili usiniombe tena siku nyingine.
“Nina uhakika watuhumiwa hawatarudia tena makosa yao, lakini nitoe tahadhari, watakaokamatwa kwa uhujumu uchumi kuanzia leo, sheria ichukue mkondo wake, isijengeke mazoea kwamba kesi ya uhujumu uchumi haipo. Siku saba nilizoongeza si kwa watuhumiwa wapya.
“Ninafahamu kuna watu wanadanganywa kuwa msamaha huu ni wa uongo. Wanadanganywa na mawakili wao ili waendelee kuwachuma fedha. Sasa waamue wao kusikiliza mawakili wao, au kukusikiliza wewe DPP na ushauri nilioutoa mimi.
“Siwezi nikafanya kazi ya kitoto, kwamba nimtege mtuhumiwa akiri, halafu kesho nitumie alichosema kama ushahidi. Nitafurahi sana kuona hao ambao tayari wamekiri makosa yao (ya uhujumu uchumi) wanatoka hata leo, waende wakaungane na familia zao.”
Tags